Wanajeshi hao waliingia mji wa Barawe
ulio kusini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu siku ya Jumatatu baada ya
kuuzingira tangu siku ya Jumapili.
Sauti za risasi zilisikika mapema Jumatau
wakati wanajeshi walikuwa wakiingia mji huo. Ripoti zinasema kuwa kwa sasa mji
huo umetulia na magari ya kijeshi kwa sasa yanapiga doria.
Mji wa Barawe haujakuwa chini ya serikali
kwa miaka 23 na umekuwa chini ya udhibiti wa al Shabab kwa miaka sita
iliyopita.
Gavana na maafisa wa kijeshi
waliwahutubia wenyeji leo ambapo walitoa wito wa kuwepo kwa utulivu wakisema
kuwa nyakati za al-Shabab zimekwisha.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini
Somalia Nicholas Kay alipongeza jeshi hilo la pamoja na kusema kuwa sasa
Somalia ina mazuri siku za usoni.
Kutwaliwa kwa mji huo ni pigo kwa kundi
la al-Shabab lililo na uhusiano na mtandao wa al-Qaeda.
Al Shabab wamekuwa wakiutumia mji huo
kupitisha silaha na chakula na pia kama kituo cha biashara ya makaa.
Muungano wa Afrika pia unasema kuwa
al-Shabab waliutumia mji wa Barawe kupanga mashambulizi yao dhidi ya mji mkuu
Mogadishu.
Chanzo: BBC Swahili
0 comments:
Post a Comment