Walter Mguluchuma, Sumbawanga.
MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Kabwe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Richard Thadeo (17) anashikiliwa na Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kuvamia ya walimu wa shule hiyo akiwa na silaha aina ya gobore na kufanya uporaji wa fedha na mali kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyopatikana jana kutoka wilayani humo, inaeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Kabwe nyakati za saa mbili usiku wakati walimu hao wakiwa nyumbani kwao wakipata mlo wa usiku.
Kwa mujibu wa Afisa Mtendaji wa Kata ya Kabwe, Joshua Mwimanzi walimu hao wawili wanaoishi nyumba moja waitwao Mwl. Izack Mwashuya na Mwl. Chrispin Kanoni wakati wakila chakula cha usiku ghafla aliingia mwanafunzi huyo aliyekuwa amevaa mavazi ya kuziba mwili na kuacha macho tu (mavazi ya kininja).
Inadaiwa kuwa mara baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, mwanafunzi huyo akiwa na silaha hiyo aliwataka walimu kumpatia kiasi cha fedha taslimu sh 300,000 kutoka kwao huku akidai kwamba 'tayari mmechukua mishahara kwa hiyo lazima tugawane" ambapo iliwalazimu walimu hao kumpatia fedha taslimu sh 75,000 na simu nne za kiganjani.
Mtendaji huyo wa kata alibainisha kwamba mara baada ya kupora vitu hivyo alitokomea kusikojulikana ndipo walimu hao walipotoa taarifa kwa uongozi wa kijiji na kata hali iliyowalazimu kuendesha msako siku iliyofuata na kufanikiwa kumtia nguvuni mwanafunzi huyo.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo wa kata, mtuhumiwa alifikishwa kwenye kituo kikuu cha polisi wilaya ya Nkasi ambako anashikiliwa kwa tuhuma ya kufanya uhalifu wa kutumia silaha na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mwanafunzi huyo anaendelea kuhojiwa na polisi wulayani humo kabla hatua zaidi za kisheria hazijachukuliwa dhidi yake.
0 comments:
Post a Comment