Saturday, December 27, 2014

MASWALI 10 KUNTU KWA MBUNGE WA KIGOMA KASKAZINI, ZITTO KABWE (CHADEMA)

 Mbunge wa Kigoma Kaskazini- Chadema Zitto Kabwe
********
1. Vumi Mbiligo, mkazi wa Msimba


Vijana wengi wamekuwa wakijishughulisha na kazi mbalimbali za kujiajiri kama vile kilimo, kuchimba mawe na mchanga, uvuvi na nyinginezo. Vijana wa Msimba walioamua kujiajiri kwa kufyatua matofali wanatozwa ushuru eti tofali ni madini. Unasemaje katika hilo na msaada wako ni nini kwa vijana?
Jibu: Ushuru wa madini hutozwa kuanzia kwenye mchanga. Ni kweli kuwa tofali ni sehemu ya madini. Lakini kwa kuwa hii ni ajira kwa vijana wetu tumeanza mchakato wa kufuta ushuru wa namna hii kwa vijana wanaojiajiri ili kuwawezesha zaidi kiuchumi.

2. Mariamu Saidi, mkazi wa Kazegunga

Halmashauri ya wilaya imekuwa na tabia ya kutoa fedha kwa vikundi vya kina mama vyenye mwelekeo wa kushabikia CCM. Unawasaidiaje wengine ambao hawana itikadi zozote za kisiasa?
Jibu: Hili katika halmashauri yetu halipo tangu nimekuwa mbunge. Tumesaidia vikundi vingi bila kujali itikadi zao. Mfano mzuri ni kina mama wa Mwandiga ambao tumewapa mtaji wa kuuza unga na hivi sasa wamepanua biashara zao kwa kiwango kikubwa. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo umejitahidi kufanya mabadiliko hayo. Iwapo kina mama wa Kagunga wamejipanga vizuri tutafanya hivyo pia.

3. Zuberi Hamisi, mkazi wa Kamara.

Wakulima wa michikichi katika Bonde la Mto Luiche hawana msaada wowote wa kitaalamu kutoka kwa maofisa ugani na hivyo kulima kizamani na kuendelea kutumia mbegu za kizamani kiasi cha kuvuna mawese kidogo. Unawasaidiaje kuwasukuma maofisa ugani kutembelea wakulima wa michikichi?
Jibu: Tunaanzisha mradi mkubwa wa michikichi katika Wilaya ya Kigoma ambao utakuwa wa mfano kwa nchi na Afrika. Kwa kushirikiana na sekta binafsi tunaanzisha ukulima wa michikichi na familia 100,000 zitafikiwa katika kipindi cha miaka mitano, zitapewa mbegu na kukuza miche 126 inayotosha kwa hekta moja. Uzalishaji huo utawezesha kila familia kuwa na kipato cha Dola za Marekani 6,000 kwa mwaka.

Mradi huu tumeuhusisha na mfumo wa hifadhi ya jamii. Kila mwanachama wa mpango huu ataandikishwa NSSF na kupata bima ya afya na kujiwekea akiba na hivyo kupata pensheni. Wakulima wa Bonde la Mto Luiche wajiandae na mradi huu kabambe kabisa ambao utakuwa ni kupigiwa mfano Afrika nzima.

4. Amisa Athumani, mkazi wa Nkungwe.

Moja ya ahadi zako tangu ulipogombea mara ya kwanza mwaka 2005 ilikuwa ni kupeleka maji Kijiji cha Nkungwe lakini hadi sasa mwaka wa tisa hakuna dalili yoyote ya kupata maji ya bomba. Una lolote la kusema kuhusu hilo?
Jibu: Mradi wa maji wa Nkungwe tayari umekamilika. Nkungwe haikuwa katika vijiji vya awali vya mradi wa Benki ya Dunia lakini nilijitahidi na kufanikiwa kuingiza kijiji hiki. Vingine ni Nyarubanda na Kagongo na vyote miradi imetekelezwa.

5. Licha ya Kijiji cha Nkunkwe kuwa kikubwa na kupata hadhi ya kuwa kata, bado kumekuwa na shida juu ya upatikanaji wa umeme wa Wakala wa NIshati Vijijini (Rea), kiasi kwamba ilifikia wananchi wakaandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma kulalamikia hilo. Nini kauli yako?
Jibu: Wananchi wa Nkungwe msiwe na wasiwasi kwani tayari umeme umefika Mahembe. Katika jimbo letu umeme wa Rea unaingia katika vijiji 16 ikiwamo Kwitanga ambayo ni sehemu ya Nkungwe. Hivyo Umeme utafika Nkungwe katika awamu inayofuata. Ikumbukwe kuwa Kigoma haikuwa sehemu ya miradi hii mpaka mwaka 2012 tulipofanikiwa kuingiza mkoa wetu. Ifikapo mwakani vijiji 20 vitakuwa na umeme kati ya 33 vya Kigoma Kaskazini.

6. Mustafa Iddi, mkazi wa Mwandiga.

Uliahidi kwamba Shule ya Sekondari Mwandiga itapanda hadhi na kutoa masomo ya kidato cha tano na sita jambo ambalo halijatekelezeka. Ina maana ulidanganya hasa ikizingatiwa kwamba umetangaza kwamba hutagombea tena katika uchaguzi wa 2015?
Jibu: Shule kuwa na kidato cha tano na sita ni mchakato. Kwanza nilianza na kuhakikisha imepata umeme na tumefanikiwa. Hatua ya pili ni kupata hadhi hiyo. Tutafanikiwa tu.

7. Kudra Hamisi, mkazi wa Kazegunga.

Umetangaza kutogombea tena Ubunge katika Jimbo lako mwaka 2015. Unawaahidi msaada gani utakaotoa kwa mgombea atakayechukua nafasi yako
Jibu: Kigoma Kaskazini ni nyumbani na nitaendelea kusaidia maendeleo yake. Mbunge yeyote atakayeshinda nitampa ushirikiano wangu wote.

8. Julius Mzega, mkazi wa Mkongoro.

Kijiji cha Mkongoro ni maarufu kwa kilimo cha nanasi lakini zao hilo limeshindwa kutatua kero za wakulima kwa vile hawana uwezo wowote wa kusindika hilo tunda. Unawasaidiaje kuleta wawekezaji watakaojenga Viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza thamani ya zao hilo la biashara na chakula?
Jibu: Kwanza tumesaidia soko kupitia mfuko wa jimbo na tunajenga soko ambalo litafanya wakulima wafaidike. Pili tunasaidia kuunda ushirika wenye nguvu na kuwezesha wakulima kujiunga na NSSF ili wapate mafao ya muda mfupi na muda mrefu. Mwaka jana nilifanya vikao na wakulima wa nanasi na tulikubaliana mambo hayo. Tunataka Mkongoro iwe ni soko kubwa la nanasi katika wilaya yetu kama ilivyo Kibaigwa hivi kwa mahindi. Dhamira ipo tushirikiane tu.

9. Isaya Samuel, mkazi wa Kalinzi.

Zao la kawana na migomba limekumbwa na magonjwa mabaya ya kunyauka. Unasaidiaje kuleta wataalamu wenye ujuzi na magonjwa hayo ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu na hatimaye kumaliza kabisa magonjwa hayo na wakulima waendelee kuvuna mazao mengi kama zamani?
Jibu: Nitasaidia kupata suluhisho. Sikuwa na taarifa hizi. Asante kwa kunijulisha.

10. Anastazia Moses, mkazi waKalinzi.

Barabara ya Mwandiga hadi Mnanila (Manyovu) ina polisi wengi wanaoomba rushwa kwa wenye magari na hata Wafanyabiashara kutokana na makosa yasiyoeleweka hivyo kufanya gharama za uendeshaji wa biashara zao kuwa kubwa. Unawapa ushauri gani ili waweze kukomesha vitendo hivyo vya rushwa katika barabara hiyo?
Jibu: Nitapambana nao. Unajua sina msalie mtume kwenye rushwa na sitaki kabisa wananchi wangu wanyanyasike. Nimepokea hili na utaona matokeo yake muda si mrefu. Lazima tuchukie rushwa kwa nguvu zetu zote kwani rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu.

Chanzo: Mwananchi:

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI