MATUMIZI
ya kondomu za kike yamekuwa changamoto kubwa baada ya wanawake mkoani Rukwa
kukataa kuzitumia, huku wengine wakibadili matumizi yake kwa kuzivaa kama
urembo wa bangili.
Hayo yalibainika hivi karibuni wakati
wa ziara ya siku nne ya timu za maofisa wa asasi mbili zisizo za kiserikali za
Health Actions Promotion Association (HAPA ) ya Mkoa wa Singida na Resource
Oriented Development Initiative (RODI) mkoani Rukwa. Maofisa hao walikuwa
wanatembelea miradi inayotekelezwa na Mradi ya Ushirikishaji wa Wanaume katika
Afya ya Uzazi na Ujinsi (TMEP) mkoani hapa.
Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali
ya Rodi inayohusika na kutoa elimu ya njia sahihi ya kutumia kondomu ili
kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), Gideon Mpina alikiri
matumizi sahihi ya kondomu za kike ni changamoto kubwa mkoani humo.
Alisema kwa kuwa kondomu hizo zina umbo
la bangili, baadhi ya wanawake wanazitumia kuvaa mikononi kama urembo kinyume
na matumizi sahihi ya kondomu hizo.
“Bangili za kondomu hizo zimekuwa
kivutio kikubwa kwa wanawake. Wanazivaa mikononi kama urembo kwani zinapendeza
machoni sababu zikipigwa na mionzi ya jua zinabadili rangi mbalimbali na kuwa
kivutio cha aina yake,” alisema Mpina.
Alisema imekuwa changamoto kubwa kwa
Rodi kwani licha ya kuisambaza bila malipo, bado baadhi ya wanawake wanazitumia
na wengine kuzinunua kutoka kwa wenzao ili tu wapate bangili.
Rodi pia inatoa elimu kuhusu malaria
mkoani hapa kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na Manispaa.
Naye Mratibu na Mfuatiliaji wa
Shidepha+ wilayani Nkasi , Anna Laurent alikiri kuwa wanawake wengi wanakataa
kutumia kondomu za kike kwa sababu wanazozijua wao wenyewe, hivyo kusababisha
kondomu hizo kudoda ofisini kwake.
“Licha ya kukataa kutumia kondomu hizi
za kike, lakini wamekuwa wakichangamkia kuchukua kondomu za kiume kwa wingi na
kusababisha uhaba mkubwa … mahitaji ya kondomu za kiume ni makubwa kwani
zinachangamkiwa na wote, wanaume kwa wanawake,” alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa
Manispaa ya Sumbawanga, Dk Richard Manumba alibainisha kuwa baadhi ya wanawake
mkoani humo hawapendi kutumia kondomu za kike, kwa sababu zinawafanya
wasiaminike na wenzao kwa kuwa baadhi yao wanadaiwa kuzitumia zaidi ya mara
moja kwa wanaume tofauti.
0 comments:
Post a Comment