Tuesday, January 26, 2016

WATU WAWILI WAFARIKI KIGOMA BAADA YA KUSOMBWA NA MAJI YA MVUA

Kigoma
Na Emmanuel Senny, Kigoma
Watu wawili wakazi wa Kata ya Kagunga kitongoji cha Zashe Mwambao wa Ziwa Tanganyika Mkoa wa Kigoma wamefariki dunia baada ya  kusombwa na maji kutokana na kunyesha mvua kubwa huku kaya tisa zikikosa makazi ya kuishi ikiwemo nyumba mbili kuangukiwa na kifusi cha mlima.
Akizungumza na Modewji Blog, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigoma, Joshua Elisha alisema kuwa, tukio hilo lilisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha Januari 22 ambapo sehemu mbalimbali mkoani hapa ziliathiriwa na mvua  ikiwemo kuharibika kwa miundombinu ya madaraja pamoja na makazi ya watu.
Alisema kuwa, waliokufa katika tukio hilo ni watu wawili ambao  walijulikana kwa jina moja moja akiwemo Kizigo (45) na Malisela (70) ila awali majina, umri na jinsia zao hazikufahamika.
“Nyumba zilizoanguka ni zaidi ya sita ikiwemo nyumba waliyokuwemo marehemu ambayo ilisombwa na maji na kusababisha vifo vyao,” alisema Elisha.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Kagunga akiwemo Nassoro Mussa ambaye ni mgambo alisema kuwa, mnamo Januari 22, mwaka huu majira ya saa 6:00 usiku mvua kubwa ilianza kunyesha hadi kuamkia Januari 23, ambapo maji yalikuwa mengi na kusababisha mafuriko na kupelekea nyumba tisa kuanguka huku nyumba mbili zilizojengwa karibu na mlima zikiangukiwa na mlima huo.
“Hadi leo tunavyozungumza zaidi ya nyumba tisa zimebomoka na wahanga wanaishi kwa majirani huku mali za wakazi wa kijiji hiki zikipotea baada ya kusombwa na maji zikiwemo  mashine sita za kuchakata  mafuta ya mawese,” alisema Mussa.
Kamanda-wa-Polisi-mkoani-Kigoma-SACP-Ferdinand-Mtui-akizungumzia-tukio-la-mtoto-kubakwa.2
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, SACP Ferdinand Mtui (pichani) alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu hao wawili baada ya nyumba waliyokuwemo kusombwa na maji ya mvua.
Aidha kunyesha kwa mvua hiyo kulisababisha miundombinu mkoani hapa kuharibika ikiwemo mradi wa chanzo cha maji kilichokasimiwa na Shirika la UN kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya ugonjwa wa kipindupindu katika kata ya Kagunga.
Miundombinu mingine iliyoharibika ni pamoja na madaraja yaliyoko katika mfereji unaopitisha maji kuelekea ziwa Tanganyika katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji ambapo serikali ya mkoa ililazimika kufunga barabara ya  Kaya Road ambayo daraja la kwa Jaffer liliathiliwa na mvua hiyo.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI