Sunday, October 5, 2014

PANYA BUKU KUTUMIKA KUKAGUA MIZIGO TANZANIA

UTAFITI mwingine kwa panya buku unatarajiwa kufanyika kuwezesha viumbe hao kunusa na kubaini harufu yenye kutoa viashiria hatari ndani ya kontena za mizigo zinazosafirishwa ndani na nje ya nchi.
Shirika la Mzinga linalomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kwa kushirikiana na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo ( Sua) na Chuo cha Antwerp cha Ubelgiji wanatarajia kuanzisha mpango mwingine wa utafiti huo.
Meneja Mkuu wa Shirika la Mzinga, Meja Jenerali Dk Charles Muzanila, alisema hayo hivi karibuni ofisini mwake alipokuwa akielezea mafanikio ya shirika kwa kipindi cha miaka 40 tangu lilipoanzishwa.
Alisema, mpango huo wa kiutafiti na kimafunzo unalenga kuwaongezea uwezo mwingine wa kunusa na kubaini iwapo kontena zina silaha na vitu vingine hatari kabla ya wapekuzi kufanya kazi kwa nia ya kubaini kilichomo kwenye mizigo husika.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Shirika hilo, mpango wa utafiti huo mpya na mafunzo hayo yatawezesha panya buku hao kupata harufu ya kitu chochote kinachonuka ama kutoa harufu fulani.
Alisema, kitendo hicho kitawezesha wataalamu wa upekuzi kufanya kazi zao za kupekua mzigo ama kontena na kupata kile kilichofichwa kwenye kontena ama vifurushi.
Utafiti huo utafanyika baada ya kupatikana kwa mafanikio makubwa ya panya buku kufundishwa namna ya kunusa na kutambua mabomu yaliyotegwa ardhini ambao walipelekwa Msumbiji kufanya kazi hiyo.
Alitaja mafanikio mengine ya panya hao ni namna walivyofanyiwa majaribio ya kimaabara ya kunusa makohozi ya binadamu kuonesha dalili za ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na kwamba tafiti hizo zinaendelea kufanyika.
Alisema Shirika la Mzinga pamoja kutekeleza mambo mengine muhimu ya kitaifa na kimataifa linajivunia kushiriki katika kutoa mafunzo ya panya buku kuweza kunusa na kubaini mabomu yaliyotegwa ardhini.
Alisema , mradi huo unaendeshwa kwa ushirikiano baina ya Sua, Chuo Kikuu cha Antwerp cha Ubelgiji,Shirika la kujitolea la uondoaji wa mabomu ya kutegwa ardhini SUA- APOPO, pamoja na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
“ Mradi wa kutegua mabomu ambao ulikuwa ni wa hatua ya kwanza katika utekelezaji wake, Shirika la Mzinga limeingia kwenye utafiti huu kwa kutengeneza miundombinu ya utafiti na kazi hii iliyofanyika kwa miaka 10 sasa imezaa matunda mazuri,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI