BAADHI ya watoto wa kike wanaosoma katika shule mbalimbali za sekondari katika Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa wanakiri kutumia uzazi wa mpango wakihofia kukatiza masomo yao kwa kupata ujauzito wakiwa bado shuleni.
Pia wanakiri kujihusisha na ngono za utotoni huku baadhi yao hata kabla hawajapevuka wakiwa na umri chini ya miaka 14.
Hata hivyo, Dk Paulo Maiga kutoka Shirika la HAPA–Singida akizungumzia madhara ya watoto wa kike wenye umri mdogo kutumia njia za uzazi wa mpango, anabainisha kuwa wanaichosha miili yao ambayo haijawa tayari kuongezewa vichocheo.
Kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini kwa kuhofia kuadhibiwa na walimu shuleni pamoja na wazazi wao, wanafunzi wanafunzi hao walikiri kutumia kwa siri njia za uzazi wa mpango ikiwemo vidonge, sindano na vijiti.
Wengine walibainisha kuwa mama zao au walezi wao wa kike wanawashauri kufanya hivyo ili kujiepusha na aibu ya kukatisha masomo kwa ujauzito.
Baadhi ya wanafunzi ambao wanaounda Klabu ya Jinsi na Ujinsi (TMEP) katika Shule ya Sekondari Kilimani, Manispaa ya Sumbawanga wanakiri kuwa baadhi ya wasichana shuleni hapo wanatumia njia ya uzazi wa mpango ikiwemo matumizi ya vidonge vya kuzuia mimba.
Wanafunzi hao walibainisha hayo wakati wa majidiliano ya wanachama wa klabu hiyo, walimu wao na maofisa kutoka Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Resource Oriented Development Initiative (RODI ) la mkoani Rukwa na Health Actions Promotion Association (HAPA) la mkoani Singida.
Mashirika hayo mawili kwa ufadhili wa Chama cha Elimu ya Afya ya Uzazi cha nchini Sweden (Rfsu) kupitia mradi wake wa Afya ya Uzazi na Ujinsia (TMEP) ambao unatekelezwa katika mikoa ya Rukwa na Singida kwa kutoa mafunzo na uhasishaji wa ushiriki wa wanaume katika afya ya uzazi na jinsia.
Mwalimu ambaye pia ni mlezi wa wanafunzi wa kike shuleni hapo, Docas Masele alieleza kuwa mihemko inayowakumba watoto katika kipindi chao cha makuzi isiwe ndio tiketi ya kujihusisha na kufanya ngono mapema.
Akifafanua, alisema kuwa visa vya ujauzito shuleni hapo vimepungua kwa asilimia 99 kwa kile alichoeleza kuwa ni baada ya kuanzishwa klabu ya TMEP shuleni hapo miaka miwili iliyopita.
Chanzo: HABARILEO
0 comments:
Post a Comment