Thursday, July 31, 2014

ZITTO AKOSA IMANI NA UKAWA: ASEMA HANA IMANI KAMA UMOJA HUO UTADUMU

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kwa mara ya kwanza ameibuka na kupingana na harakati za Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA). 
Zitto amesema hana uhakika wala hauamini Ukawa kama utakuwa umoja endelevu hadi kufikia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwa sababu si mara ya kwanza vyama vya upinzani kuungana na kugawanyika. 
Mbali ya kutokuwa na imani na umoja huo, pia ameitaka Serikali kusitisha mchakato wa Katiba Mpya hadi uchaguzi mkuu utakapomalizika. 
Alisema ni vema mchakato huo ukasitishwa kwa sasa, kwani inaonekana wajumbe wa Bunge hilo wanafuja fedha za umma.
Zitto alitoa kauli hiyo juzi, wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds cha jijini Dar es Salaam.
Alisema Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi na si Katiba pekee.
Alisema siku zote Watanzania wamekuwa wakipenda kuwa na upinzani imara ambao watu wanaweka tofauti zao pembeni na kuungana dhidi ya chama ambacho kinaongoza, lakini haoni kama Ukawa utaendelea hadi kufikia kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
Alisema hatua ya kusimama kwenye ajenda moja ya Katiba haitausaidia umoja huo, kwani kipindi cha uchaguzi mkuu kinakuwa na ajenda nyingi.
Alisema wananchi watapenda kusikia masuala ya kushughulikia rushwa, matumizi ya rasilimali, maji, umeme, afya na barabara.
“Mambo haya ndiyo yatakayowafanya wananchi waamue namna gani watakabidhi dhamana ya uongozi, si suala la Katiba pekee,” alisema Zitto.
Alisema tusijitoe ufahamu kwa kudhani kwamba hii ndio mara ya kwanza kwa upinzani kuungana. 
“Kulikuwa na Kamati ya Mabadiliko ya Katiba (KAMAKA) pia katika chaguzi za mwaka 1995, mwaka 2000 wapinzani waliungana vilevile, lakini kila inapokaribia uchaguzi wamekuwa hawaelewani kwa kuwa kila mtu anataka chama chake kipeperushe bendera.
“Lakini kama Ukawa wataweza kuweka ajenda yao mpaka mwisho itakuwa jambo jema kwa wananchi wenyewe. Kwa sababu nchini kwetu tatizo kubwa ni usimamizi na uwajibikaji, kama ajenda itachukua nafasi naamini hali haitakuwa mbaya, lakini bado siamini na sina uhakika kama umoja huu ni endelevu kwa namna ambavyo tunaona, ni umoja ambao unatokana na matakwa ya sasa ya Katiba, wameungana kwa sababu ya serikali tatu, lakini aina gani ya serikali bado hili linaweza kuwagawa,” alisema.
…MCHAKATO WA KATIBA MPYA USITISHWE...
Akitolea ufafanuzi hoja yake ya kusitisha mchakato wa Katiba Mpya, Zitto alisema ni vyema serikali ikausitisha ili kunusuru fedha za umma zisiteketee.
Alisema fedha hizo zinastahili kutumika kununua madawa, kuendeleza miradi ya maji na kusomesha Watanzania, hivyo hakuna sababu fedha hizo kutumika kwa ajili ya kupiga porojo na kutukanana ndani ya Bunge.
“Nashauri tuahirishe mchakato huu mpaka baada ya uchaguzi mkuu mwaka kesho, ndipo hapo tuwe na mamlaka ya kujadili mchakato huu na kumaliza.
“Pia uchaguzi unaweza kuchekecha na ukaondoa baadhi ya watu ambao ni vikwazo katika mchakato kwa sababu uchaguzi hauna muamala, mtu ambaye alikuwa mbunge anaweza kuondolewa,” alisema.
Aidha, alisema kabla ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu, Katiba ya sasa inatakiwa kurekebishwa baadhi ya maeneo ambayo ni vikwazo, kama vile Tume huru ya uchaguzi, kipengele cha wagombea binafsi kiwekwe na maeneo ambayo Zanzibar wamekuwa wakiyahitaji katika Katiba mpya, kwa mfano suala la mafuta na gesi yawekwe.
Alisema hakuna sababu ya kugawa nchi na kutumia rasilimali zilizopo kwa kufanya kazi ambayo haina matunda.

…AMTETEA JANUARY...
Katika hatua nyingine, Zitto, ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, alisema amesikitishwa na mashambulizi yanayoelekezwa kwa Mbunge wa Bumbuli (CCM), Januari Makamba, baada ya kutangaza nia ya kuwani urais mwaka 2015.
Mbunge wa Bumbuli, Mhe. January Makamba (CCM).
Alisema kila kijana anapojitokeza kwa ajili ya kutaka kushiriki katika mamlaka za nchi, hasa katika nafasi kama hiyo ya urais, kumekuwa na mashambulizi makubwa dhidi yake.
“Ni hatua ambayo sio nzuri kwa sababu kwa mujibu wa takwimu, idadi ya watu asilimia 72 wapo chini ya miaka 30, asilimia 65 ya wapiga kura ni vijana wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 40, hivyo vijana wana haki ya kushiriki katika uongozi wa nchi, tufahamu changamoto za maendeleo ya nchi yetu zinahitaji uongozi mpya wa kizazi kipya.
“Ni dhahiri neno ujana si sifa, lakini neno uzee pia si sifa, hivyo tunatakiwa kuwapima vijana kwa sifa zilizopo, kama vile za kikatiba na zile za ziada, badala ya kusema vijana hawajakomaa… nilisikitika sana na mashambulizi ambayo yalielekezwa dhidi ya Makamba, natoa wito kwamba tuache, kwani wenye uamuzi wa mwisho ni wananchi.
“Mtu akigombea na kama akitoa sera zake vizuri wananchi wakamwelewa, akichaguliwa ni wananchi wameamua, hakuna mtu mwenye mamlaka kuwa fulani ni kijana, nadhani lazima tubadilishe uongozi na watu wajue nchi hii ni ya vijana, hatusemi wazee hawawezi ila wao wabaki kuwa washauri kama wao walivyokuwa vijana katika kipindi cha Nyerere nao walikuwa na miaka 40. Hivyo kuna haja ya kuweza kufikia hapo, changamoto za nchi ni kubwa, kuna haja ya aina mpya ya uongozi na mimi naamini aina hiyo itatoka kwa viongozi vijana,” alisema.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa Zitto, ambaye yuko ndani ya Chadema kwa sababu za kisheria, kuibuka na kuuzungumzia Ukawa.
Mwanasiasa huyo kijana amekuwa kimya kwa muda mrefu, hata kwenye harakati za Ukawa amekuwa aghalabu kuonekana, hali ambayo imekuwa ikiibua maswali yuko upande gani katika mchakato huu wa Katiba Mpya.
Kauli hii ya Zitto inaweza kuibua fikra mpya kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa na imani kubwa na umoja huo unaoviunganisha baadhi ya vyama vya siasa nchini.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI