Sunday, May 25, 2014

LIGI YA MABINGWA: AL AHLY BENGHAZI, ZAMALEK ZASHINDA, SAMATA, ULIMWENGU KUIONGOZA TP MAZEMBE DHIDI YA AS VITA MJINI LUBUMBASHI

Zamalek walishinda
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
LIGI ya mabingwa barani Afrika hatua ya makundi iliendelea jana kwa mechi mbili kupigwa katika nchi mbili tofauti.
Al Ahly Benghazi ya Libya ikiwa nyumbani iliibuka na ushindi mabao 3-2 dhidi ya Esperance ya Tunia.
Mchezo mwingine ulipigwa nchini Misri ambao wenyeji Zamalek waliichapa Al Hilal ya Sudan mabao 2-1.
Ligi hiyo itaandelea leo kwa mechi mbili kupigwa katika nchi mbili tofauti.
Nchini DR Congo, washambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samata na Thomas Emmanuel Ulimwengu wataiongoza TP Mazembe mjini Lubumbashi kuwakabili mahasimu wao wa jadi, AS Vita ya DR Congo.
Hii ni mechi inayovuta hisia za mashabiki wengi barani Afrika kutokana na upinzani unaokuwepo mara timu hizi zinapokutana, iwe katika ligi ya ndani au mashindano ya kimataifa.
Majembe: Kila la heri vijana wetu Samata na Ulimwengu katika mchezo wa leo.
Wiki za karibuni, TP Mazembe na AS Vita walikutana katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya DR Congo mjini Kinshasa na vijana wa Moise Katumbi kuibuka na ushindi wa bao1-0.
Hata hivyo mchezo huo uliingia katika historia mbaya baada ya kutokea vurugu kubwa za mashabiki na kusababisha vifo vya mashabiki zaidi ya 15.
Hakika tukio hili lilikuwa baya katika ulimwengu wa soka, lakini chanzo chake ni mashabiki wa AS Vita kukosa uungwana na kushindwa kukubali matokea.
Hofu imetanda mjini Lubumbashi kwasababu siku za nyuma iliripotiwa kuwa mashabiki wa Mazembe wanaweza kulipa kisasi kwa kile walichofanyiwa mjini Kinshasa.
Lakini taarifa kutoka nchini Congo zinaeleza kuwa usalama utaimarishwa wakati wote wa mchezo na kwa bahati nzuri hakuna rekodi ya vurugu katika uwanja wa Mazembe kama ilivyo kwa AS vita.
Wadau wa michezo wanaombea amani katika mchezo huo na Mazembe wasilipize kisasa kwa AS Vita.
Mechi nyingine itapigwa nchini Algeria ambapo wenyeji ES Setif watakabiliana na SC Sfaxien kutoka nchini Tunisia.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI