Wednesday, November 2, 2016

HATUA ILIZOCHUKUA BURUNDI BAADA YA WAFADHILI KUKATA MISAADA

Baada ya nchi za magharibi zinazofadhili Burundi kuonesha kutopenda hatua ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kuwania Urais kwa muhula wa tatu, pamoja na kutumia nguvu kuzima maandamano na hivyo kukata misaada iliyokuwa wakitoa kwa nchi hiyo.
Habari iliyoripotiwa na BBC imeeleza kuhusu hatua mbalimbali ambazo nchi hiyo imezichukua baada ya wafadhili kukata misaada, Taarifa zinasema kwamba kuanzia sasa katika mji mkuu wa Burundi waendeshaji baiskeli, Pikipiki na magari wataanza kulipa ada ya kuegesha.
Serikali inanuia kukusanya mapato zaidi baada ya wafadhili wa magharibi kukata msaada wake kwa nchi hiyo. Aidha imeelezwa kuwa Serikali imefuta ufadhili wake kwa Vyuo Vikuu na badala yake wanafunzi wote watagharamia ada za masomo punde wakiajiriwa baada ya kufuzu.
Ada mpya za kuegesha ni dola mbili sawa na takribani Tsh 4,300 kwa baisikeli na dola 60 sawa takribani Tsh 130,000 kwa malori makubwa. Mabasi ya umma yatalipa dola sita sawa na takribani Tsh 13,000 kwa mwezi. Raia wengi wanahofia ada mpya huenda zikasababisha mfumuko wa bei ya bidhaa. Wakazi wengi katika mji mkuu tayari wanalalamikia ongezeko la gharama ya maisha huku ikielezwa kuwa wafanyakazi wengi hupokea dola 80 kwa mwezi.
Muungano wa Ulaya ulisimamisha msaada kwa serikali ya Burundi na kusema Mamlaka hazijasaidia kurejesha utulivu nchini.Msaada wa Muungano wa ulaya kwa Burundi ulikadiriwa kuwa dola milioni 470 kati ya mwaka 2014 hadi mwaka 2020.
Zaidi ya watu 400 wameuawa na wengine laki mbili na nusu kukimbilia katika nchi jirani kufuatia machafuko ya kisiasa yaliyozuka baada ya Rais Nkurunziza kuamua kuwania muhula wa tatu.
Mwezi uliopita Burundi ilitangaza kujiondoa kutoka uwanachama wa mahakama ya kimataifa ya jinai ICC. Tangazo hili lilitolewa miezi sita baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa ICC kusema atachunguza ghasia nchini humo.
#BBC

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI