Sunday, March 6, 2016

BAADA YA NDOA MKE WA DR SLAA AFUNGUKA....'HAIKUWA RAHISI KUFUNGA NDOA NA DK SLAA TUMEPITIA MENGI'

Baada ya kuenea taarifa za Dk Willibrod Slaa kufunga ndoa na mchumba wake wa siku nyingi, Josephine Mushumbusi, mwanamke huyo ameibuka na kuthibitisha huku akisema haikuwa kazi rahisi kufanikisha jambo hilo.

Dk Slaa na Mushumbusi walifunga pingu za maisha Februari 26 katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Merciful Redeemer, Canada na mwanamke huyo amelieleza gazeti hili kuwa, mchakato wa kufungwa kwa ndoa hiyo uliwachukua muda mrefu na kupitia vikwazo vingi.

Wanandoa hao waliondoka nchini kwenda Marekani Septemba mwaka jana, siku chache baada ya katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema kujiuzulu uongozi na kujivua uanachama wa chama hicho na kuachana na siasa za vyama. Baadaye walihamia Canada wanakoishi hadi sasa.

Akizungumzia ndoa yao, Mushumbusi alisema ilikuwa ngumu kufungwa, lakini walipambana na kutimiza taratibu zote na kuifanikisha.

“Tunampa Mungu sifa na utukufu, haikuwa rahisi. Tumefuata taratibu zote na kufunga ndoa takatifu kanisani kama tulivyotamani,” alisema.

Ndoa hiyo ilifanikiwa baada ya kukwama hapa nchini Julai 21, 2012 kutokana na pingamizi la mke wa zamani wa Dk Slaa, Rose Kamili na mgogoro ulitokana na aliyekuwa mume wa Mushumbuzi, Aminiel Mahimbo.

Mushumbusi alisema iliwachukua muda mrefu kukubaliwa kufunga ndoa kutokana na taratibu za Canada ambazo ziliwataka wapate mafunzo kwanza, wathibitishwe kuwa hawakufunga ndoa kabla na kuwasilisha tangazo maalumu la kustaafu upadri wa Dk Slaa.

Alisema Canada siyo rahisi kufunga ndoa bila kibali cha Serikali na kukipata ni mchakato mrefu.

“Tumevumilia na kukamilisha yote hayo, siyo kama nyumbani ambako ni rahisi kufanyika, watu wanawaza sherehe huko Tanzania lakini huku unaumiza kichwa kupata vibali vya kanisa na Serikali,” alisema.

Ndoa ya Mushumbusi na Dk Slaa ilisimamiwa na wanandoa raia wa Canada aliowataja kwa jina mojamoja la Rosemary na Emmanuel na mashuhuda kadhaa kutoka Tanzania ambao hakutaka kuwataja.

Awali, kulikuwa na taarifa kuwa wawili hao hawakufunga ndoa katika Kanisa Katoliki kutokana na kushindwa kutimiza kanuni na taratibu, lakini Mushumbusi alisema ndoa hiyo imefungwa kanisani na kupata baraka zote. Akizungumzia maisha ya huko Mushumbusi alisema kwa sasa Dk Slaa anasoma na baada ya kumaliza masomo hayo watarejea nyumbani.

Azungumzia uchaguzi
Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, Mushumbusi alisema alifurahia Rais John Magufuli kushinda kwa kuwa anayajua madhara ya Ukawa kushinda chini ya Edward Lowassa.

“Si unaona Ukawa wanalalamika majipu kutumbuliwa, niliyajua madhara kama hayo ndiyo maana nimeshukuru Magufuli kushinda,” alisema.   

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI