Saturday, November 28, 2015

TRA YAANZA KUNG’ATA, WAFUNGA SAPNA, WAKAMATA MAGARI UDA KISA? IPO HAPA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA), imeanza operesheni maalumu ya kunasa wafanyabishara wakubwa ambao wengine ni wadaiwa sugu ambapo wanadaiwa na mamlaka hiyo huku wafanyabishara wa duka la simu la Sapna lililopo eneo la Posta mpya jijini Dar es Salaam likitiwa kufuli.
Operesheni ya TRA dhidi ya wanaodaiwa fedha ilianza jana maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambapo maofisa wa mamlaka hiyo walikuwa wanakwenda eneo moja hadi jingine na kote ambako wamekwenda wamefunga ofisi za wafanyabishara hao.
Maofisa wa TRA waliokuwa na nyaraka mbalimbali za madeni walipokuwa wanafika kwenye maeneo ya wafanyabishara hao hawakuwa na muda wa kupoteza zaidi ya kufunga ofisi huku baadhi ya maofisa hao walikuwa wakisema kuwa Hapa Kazi Tu.
Duka la Sapna ililifungwa jana saa tisa alasiri ambapo maofisa wa TRA ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao walidai kuwa wamiliki wa duka hilo ni miongoni mwa wanaodaiwa na TRA na tena ni kiasi kikubwa cha fedha.Hata hivyo hawakutaja kiwango halisi cha fedha huku wakifafanua kuwa wamiliki wa duka hilo walipewa taarifa mapema, hivyo hawakuvamia zaidi ya kutumia utaratibu maalumu.
Wakati duka hilo linafungwa wananchi walikuwa eneo hilo walijikuta wakishangaa kuona namna ambavyo wamiliki wa duka hilo wenye asili ya Asia wakibaki wameshika vichwa bila kujua la kufanya. Moafisa wa TRA mbali ya kufunga duka hilo, pia waliamua kufunga gari la mmoja wa wamiliki wa duka hilo.
Mbali ya kufunga duka hilo pia maofisa wa TRA walikwenda kwenye ofisi za Shirika la Usari Dar es Salaam (UDA), ambako nako wamekamata baadhi ya magari kutokana na kudaiwa kodi huku pia ikielezwa eneo lingine ambalo mamlaka hiyo imefanya operesheni ni eneo la Victoria ambapo kuna kampuni inayohusika na uuzaji wa redio upepo na rimoti za magari
. Kwenye eneo hilo magari manne yamechukuliwa na TRA.
Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa wa TRA ni kwamba operesheni hiyo itaendelea tena leo huku pia ikielezwa kuna viwanda mbalimbali ambavyo vimefungwa kwa kushindwa kulipa kodi. Hata hivyo alipotafutwa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi TRA Richard Kayombo kuzungumzia operesheni hiyo hakupatikana.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI