RAIS John Magufuli amemtumia salamu za pole Rais wa Ufaransa François Hollande, kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyogharimu vifo vya watu 127.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Rais Magufuli alisema Serikali yake inaungana na wapenda amani wote duniani kulaani tukio hilo lililogharimu maisha ya watu wengi.
Awali taarifa za AFP zilisema serikali ya Ufaransa iko kwenye hali ya tahadhari baada ya kutokea mashambulizi mfululizo ya kutisha kufanywa kwenye maeneo maarufu jijini Paris Ijumaa usiku na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 127.
Tayari kikundi cha wanamgambo wa ISIS kimeshasema kimehusika na mashambulizi hayo.
Waliofanya mashambulizi hayo walilenga maeneo mepesi kufikika ambako watu walikuwa wakiendelea kusherehekea wikiendi kwenye eneo ambalo hufanyika matamasha ya sanaa, mahoteli na baa, na kwenye Uwanja wa Taifa wa Ufaransa ambako mechi ya kimataifa ya soka ilikuwa ikichezwa.
Ikiwa imeshatingishwa na shambulizi la kigaidi la Januari, jiji la Paris lilikumbwa na kiwewe na hali ya kuchanganyikiwa.
“Ni kama Paris imetekwa kwa sasa,” alisema mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha CNN, Anne-Charlotte Hinet baada ya watu hao kushambulia maeneo sita kwenye jiji la Paris.
Mamlaka ziliwataka wananchi kutotoka nje, huku Jiji likiwa limefunga majengo mengi ya umma na kuongeza ulinzi wa kijeshi.
Mashuhuda walisema kwenye eneo linachukua zaidi ya watu 1,500 ambako tamasha la muziki lilikuwa linafanyika, walieleza jinsi washambuliaji hao walivyokuwa wakifyatua risasi kuelekea kwa watu.
Mlipuko uliotokea karibu na uwanja wa michezo wa Stade de France, ambao umeelezewa kuwa ulikuwa wa kujitoa muhanga, ulikuwa wakati timu za taifa za Ujerumani na Ufaransa zikicheza, na kusababisha Rais Francois Hollande kuondolewa uwanjani.
0 comments:
Post a Comment