Monday, September 21, 2015

WENGI WAMZIKA MTOTO WA KIONGOZI WA WAFUGAJI LUGOBA, RAIS ATUMA RAMBIRAMBI

unnamed (78)
Baadhi ya waombelezaji katika msiba huo. Kulia ni Ridhiwani Kikwete mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia CCM akifuatiwa na mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga, mkuu wa wilaya ya Nachingwea Pololet Mgema na mgombea ubunge Jimbo hilo kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Matayo Torongei wakiwa kwenye msiba huo.

Na John Gagarini, Lugoba 
Wagombea wa nafasi za uongozi hapa nchini wametakiwa kukubali matokeo mara uchaguzi utakapofanyika Oktoba 25 mwaka huu kwani kuna maisha mengine baada ya uchaguzi, na   kuendelea kufanya kampeni zao huku wakiendelea kuhubiri na kulinda amani iliyopo kwani wana nafasi kubwa ya kuwashawishi wafuasi wao wasifanye vurugu au kufanya vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa amani. 
 Pia wagombea watakaoshindwa kwenye uchaguzi mkuu wameombwa wakubali matokeo kwani kwenye washindani lazima kuwe na washindwa ili kuondoa hali ya mafarakano kwani kwa wale watakaoshindwa wasipokubali matokeo wanaweza kuleta uvunjifu wa amani. 
 Hayo yalisemwa katika  Kijiji cha Maviayangombe kata ya Lugoba wilayani Bagamoyo mkoani
Pwani na Askofu mkuu wa Dayosisi ya Morogoro ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jacob Mameo Ole Paulo wa Dayosisi ya Morogoro wakati wa mazishi ya mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa wafugaji Laban Moreto, Karokya Moreto (33) ambaye alikuwa mwanajeshi wa kikosi cha 04/691 cha Mtwara. 

 Askofu Ole Paulo alisema kuwa wagombea hao wanauwezo wa kudumisha amani kwa kuhubiri au kuingiza nchi kwenye machafuko endapo watayatumia vibaya majukwaa wakati wa kipindi hichi cha kampeni za uchaguzi. 
 “Wanapaswa kuhubiri amani na kuacha kutumia maneno yatakayo haribu amani ya nchi iliyopo ambayo imedumu kwa kipindi kirefu tangu nchi ilipopata uhuru miaka zaidi ya 50 hivyo itakuwa ajabu ivunjwe kisa kuwania uongozi tu,” alisema Askofu Ole Paulo. 
Alisisitiza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kupingana kwa hoja na kwa malumbano ambayo hayana maana bali yanaweza kuleta mitafaruku isiyokuwa ya lazima hasa kwa wale wanaoshindwa kwani wanapaswa kukubali matokeo. 
 Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alisema kuwa amesikitishwa na kifo cha marehemu ambaye alikuwa ni ndugu kwani wamekuwa wakiishi kama familia moja na walikuwa na ushirikiano mkubwa baina ya familia zao. 
 Ridhiwani alisema kuwa kifo hicho ni pigo kwa familia hiyo pia kwa Taifa kwani alikuwa ni mtumishi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na alikuwa mtaalamu wa rada hivyo pengo lake haliwezi kuzibika kikubwa ni kumwombea marehemu. 
Rais Dk Jakaya Kikwete alituma salamu za pole kwa familia hiyo kupitia kwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete na kusema kuwa anatoa pole na Mungu awape nguvu katika kipindi hichi kigumu cha maombolezo na yuko pamoja nao. 
 Alisema kuwa Rais alishindwa kuhudhuria msiba huo kwani kwa sasa yuko nje ya nchi lakini pindi atakaporudi ataitembelea familia hiyo kwa ajili ya kuifariji kufuatia kifo cha mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa kabila wafugaji 
 Naye mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mathayo Torongei alisema ili amani iendelee kuwepo ni vema dola ikatenda haki badala ya kupendelea upande mmoja. 
 Marehemu alifariki kwa ajali baada ya gari alilokuwa akiendesha kupasuka tairi la mbele na kusababisha ajali iliyopelekea kifo chake siku ya Septemba 16 mwaka huu huko Mtwara. Ameacha mke na watoto watatu.
unnamed (79)Askofu Jacob Mameo Ole Paulo akizungumza wakati wa msiba huo.
unnamed (74)Jeneza lenye mwili wa marehemu likiwa limebebwa na wanajeshi ukiwasili makaburini
unnamed (77)Baadhi ya Wazee wakiwa wamekaa kwenye msiba huo huko kijiji cha Maviyangombe Lugoba wilayani Bagamoyo.
unnamed (73)Baadhi ya akinamama ambao ni ndugu wakaribu wakilia.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI