Monday, September 21, 2015

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) YATUPILIA MBALI MALALAMIKO YA MBOWE

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imepuuza malalamiko ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) juu ya kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Abdallah Bulembo, kuwa chama chake hakitakuwa tayari kuiachia Ikulu kwa namna yoyote ile, ikisema ni ya kisiasa na hayana madhara yoyote.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, amesema kwa sasa kila chama kipo kwenye kampeni za kutafuta ushindi, hivyo kauli kama hiyo inaweza kutolewa na upande wowote ikiwa ni mbinu ya kujipatia ushindi.

“Ingekuwa kauli yake tafsiri yake ni kuwa hawatakubali matokeo ya uchaguzi hapo tume ingekuwa imehusika na ingezungumza kwa kuwa tulishasema kila chama shindani katika uchaguzi huu kinatakiwa kukubali matokeo yatakayotangazwa na tume,” alisema.

Alisema hadi sasa NEC haijaona cha kujibu juu ya kauli hiyo na inaichukulia ni matamshi ya kisiasa ya kampeni.

Hivi Karibuni Bulembo akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika mjini Kigoma, alidaiwa kutoa kauli kuwa chama chake hakitakuwa tayari kuiachia Ikulu kwa namna yoyote ile.


Mwenyekiti wa Ukawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akizungumza na waandishi wa habari, juzi alilalamikia kauli hiyo na kuitaka NEC kulaani kauli hiyo kwa kuwa uchaguzi ni ushindani na hakuna mwenye maamuzi zaidi ya wapiga kura.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI