Monday, July 6, 2015

MMEACHANA? HAKUNA SABABU YA KUCHUKIANA!

Mpenzi msomaji wa XXLove karibu kwenye Jumatatu nyingine mwanana katika ulimwengu wa uhusiano wa kimapenzi.Katika mada yetu tajwa hapo juu, nitazungumza na wale rakifi zangu walioachana au kuachwa na kuanza kumchukia mwenza wake.  
Ni kweli kuachwa kunaumiza sana moyo. Kimsingi usiombe kukumbwa na maumivu ya kuachwa. Lakini kama hilo limekwishatokea, kwa nini uendelee kuumia na kumchukia aliyekuwa mpenzi wako?
Kitendo cha kukuacha wewe, kinaweza kumtokea hata yeye na kujikuta akilia na kuhuzunika kama wewe. Kama ndivyo basi mapenzi ndivyo yalivyo. Leo kwako, kesho kwake.
Hakuna sababu ya kuchukiana na kuwekeana visasi kwa sababu kama tutafanya hivyo, kwa dunia ya sasa iliyojaa uchepukaji, itakuwa dunia ya visasi kila kukicha.
Ifahamike kwamba, mapenzi hayana fomula, inawezekana mwenza wako akawa amerubuniwa na kuna siku atarejea kwako na kutulia kama unavyotaka.
Siwatetei wenye tabia ya kuacha, wala siyo tabia nzuri kubadilisha wapenzi, lakini pengine ni ujana ndiyo unamsumbua au ni tabia asili ya mwenza wako, tabia ambayo haipaswi kuigwa na ni hatari kiimani, kimaadili na hata kiafya.
Ninavyofahamu mapenzi ni kitu cha ajabu sana, inawezekana mkawa mmeachana kwa muda kwa maana ya kupumzishana au kuna mtu kaingilia kati penzi lenu au mmeachana moja kwa moja.
Haijalishi ni aina ipi ya kuachana ila ninachozungumzia ni kuachana au kuachwa na kujenga chuki, hakuna sababu kwa namna mapenzi yalivyo kwa sababu utachukia wangapi? Hivi kwa mfano, ukiachwa au kuachana na wapenzi watano na wote ukawachukia, si utakuwa umetengeneza bomu la hatari katika maisha yako? Kwa sababu utakuwa ukiwaona moyo wako unaumia na kuwaza mabaya juu yao.
 
Kama mlikuwa mnajua mtakuja kugombana, hamkuwa na sababu ya  kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na kama mlilazimishana, kupendana hakuna sababu ya kuchukiana. Naamini hamkujua kama mtakuja kugombana ndiyo maana mliamua kupendana na ‘kushea’ baadhi ya vitu vyenu.
Sidhani kama mliamua kuwa wapenzi ili mje kupeana stress (msongo), mgombane, mchukiane, muharibiane maisha na mambo mengine.
Kama umeachwa kwa sababu za msingi, kubaliana na ukweli ili maisha yasonge kuliko kuendelea kufikiria na kutengeneza chuki na uhasama na mtu aliyekuacha au kuachana, haisaidii kitu, kama wewe unavyohisi kutendwa na yeye huko alikokwenda anaweza kutendwa vilevile. Mapenzi ni mchezo usiokuwa na bingwa.
Angalizo; kwa wale wenye tabia ya kuacha hovyo, haipendezi kwani kuna mambo mengi ambayo unaweza kuyatengeneza bila kujua.
Wanawake huamini kwamba unapomuacha, huwa umemchezea kwa maana ya kutimiza haja zako na unapopata mtu mwingine ‘unamshiti’ bila kujua kuwa uhusiano wa mapenzi ni kama kitabu ambacho kinapaswa kifunuliwe kurasa zake. Inawezekana anayekifunua, akafunua kurasa moja na kukutana na andiko alilokusudia au kufunua kurasa zaidi na zaidi.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI