Thursday, February 19, 2015

COASTAL UNION WAIFUATA NDANDA MTWARA


Na Mwandishi wetu, Tanga.
TIMU ya Coastal Union ya Tanga imeondoka mkoani hapa leo asubuhi kuelekea mkoani Mtwara kwa ajili ya mechi yao ya Ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda SC itakayochezwa  Jumamosi wiki hii. 
Coastal Union ambayo mechi yao iliyopita dhidi ya Mbeya City iliyochezwa kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani haikupata matokeo mazuri sana baada ya kulazimishwa sare hivo itaingia kwenye mechi Hiyo mithili ya mbogo aliyejeruhiwa msituni.

Akizungumzia maandalizi ya kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Mkenya James Nandwa alisema kuwa kikosi chake kimeimarika zaidi baada ya kuyafanyia kazi kwa asilimia kubwa mapungufu yaliyojitokeza mechi iliyopita.

Alisema kuwa dhamira yake kubwa ni kuhakikisha kikosi hicho kinaibuka na ushindi kwenye mchezo huo ambao unatazamiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na kila timu msimu huu kuonekana Kujiimarisha vilivyo kwa ajili ya kupata matokeo mazuri.

  "Kikosi changu kipo imara kuweza kuwakabili Ndanda SC ikiwemo kuhakikisha tunapata  matokeo mazuri hii inatokana na maandalizi kabambe tuliyoyafanya hasa kubwa kurekebisha  baadhi ya maeneo kwenye kikosi hiki "Alisema Kocha Nandwa.

Alisema kuwa mipango yake hivi sasa ni kukiwezesha kikosi cha timu hiyo kuweza kufanya  vizuri kwenye mechi zao zijazo ili kuweza kusogea kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa  Ligi kuu hapa nchini. 

Msafara wa Coastal Union uliondoka leo (19/02) mkoani hapa kuelekea mkoani Mtwara unaongozwa  na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ,Albert Peter ambapo baada ya kuwasili mkoani mtwara  utafanya mazoezi.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI