MWANAFUNZI wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 13 wa shule ya msingi ya Themi iliyopo jijini Arusha mkoani Arusha hali yake siyo nzuri baada ya kubakwa na watu sita.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 1 usiku Oktoba 7 mwaka huu katika kata ya Daraja Mbili jijini Arusha. Imeelezwa kuwa sehemu yake ya kizazi imeharibika kutokana na unyama huo.
Akizungumza na mwandishi jana nyumbani kwake Daraja Mbili mara baada ya kuruhusiwa kutoka katika Hospitali ya Kanisa Katoliki ya Father Babu ya jijini na kuendelea na matibabu Hospitali ya Serikali ya Mount Meru Arusha mwanafunzi huyo alisema pamoja na kuruhusiwa kutoka hospitali lakini hawezi kutembea kutokana na maumivu makali yanayomsumbua.
Alisema siku hiyo kulitokea ugomvi nyumbani na mama yake Zukhura Said (40) na aliamua kukimbilia kwa mjomba wake ndipo njiani alipokutwa na dhahama hiyo ambayo katika maisha yake hataisahau.
Mwanafunzi huyo alisema alifanyiwa unyama huo karibu sana na nyumbani kwao na watu waliomfanyia unyama huo anawafahamu kwa majina na sura na watatu wameshakamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha na watatu bado hawajakamatwa.
Mwanafunzi huyo akizungumza alisema wakati akifanyiwa unyama huo alipoteza fahamu na alijikuta asubuhi akiwa nje ya chumba cha mmoja wa watuhumiwa hao.
‘’Nimefanyiwa unyama mkubwa sana nilipoteza fahamu kutokana na unyama huo na kwa mujibu wa daktari kizazi changu kimetoboka shangazi yangu ndio aliyepiga simu nyumbani kujulisha hali hiyo kwani alinikuta hapo nje asubuhi majira ya saa 2 asubuhi’’, alisema mwanafunzi huyo.
Akizungumzia tukio hilo mama mzazi wa mtoto huyo, Zukhura Said (40) alisema anasikitishwa na jinsi upelelezi wa tukio hilo unavyoendeshwa kwani mpelelezi wa tukio hilo {jina tunalo} amekuwa mstari wa mbele kutaka wazazi wa pande zote wamalizane kwa kukaa mezani.
Mama huyo alisema wahalifu waliosalia wako mtaani na wazazi wao kwa kushirikiana na kiongozi wa mtaa {jina tunalo} wanafanya kila njama na fitina kutaka kesi hiyo iondolewe Polisi na kurudishwa nyumbani.
0 comments:
Post a Comment