Waasisi wa Muungano wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (kushoto) na Hayati, Abeid Aman Karume (kulia waliokaa) wakisaini nyaraka muhinchi za Hati za Muungano mwaka 1964 (mada ya historia).
******************************
''WASOMI NA WANASIASA WAKONGWE NINYI NDIYO HASA TEGEMEO LA KWELI KWA VIJANA WA KIZAZI KIPYA KWA KUMBUKUMBU MLIZONAZO KUHUSU SUALA ZIMA LA TANGANYIKA NA ZANZIBAR, BADALA YAKE MNAWALISHA SUMU VIJANA ILI KUAMINI KILE MNACHOKIELEZA MBELE YA JAMII, MNAHISI NINI KITATOKEA IWAPO VIJANA WA DOT COM WAKIAMINI MNACHOKIPIGIA DEBE???? BADALA YA KUUELEZA UMMA UKWELI NA KUJENGA HOJA YA HAJA ILI MUWEZE KUELEWEKA''.
Rais Julius Kambarage Nyerere, akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar, huku akishuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Abeid Aman Karume, (wa tatu kushoto) na Mhe. Rashind Mfaume Kawawa (wa kwanza kulia) wakati wa sherehe za kwanza za Muungano zilizofanyika Tarehe 26 APRIL, 1964.
|
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (kushoto) na Sheikh Abeid
Amani Karume (kulia) wakibadilishana Hati za Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar mwezi Aprili, 1964.
|
Walioshiriki katika tukio la kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 24 Aprili, 1964 wakiwa katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam wakati wa halfa fupi ya sherehe za miaka 48 ya Muungano tarehe 26 Aprili, 2012. Kutoka kushoto ni Bi. Khadija Abasi Rashid, Bw. Elisaeli Mrema, Bw. Hassan Omari Mzee na Bi. Sifael Mushi.
Rais Julius K. Nyerere (katikati), Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Rais wa Zanzibar Mhe. Abeid Amani Karume wakukagua gwaride wakati wa maadhimisho ya sherehe za Muungano zilizofanyika Zanzibar mwaka 1966.
*********************************************
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU HATI ZA MUUNGANO
TAREHE 14 APRILI, 2014
__________________________
Siku 12 zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamezaliwa watu ndani ya Muungano huu na wengine wana wajukuu.
Inasikitisha sana kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu inayojengwa kuwa Muungano huu si halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano (Articles of the Union).
Waasisi wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia saini Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.
Mambo yote mawili yametusononesha sana sisi Serikalini, na bila shaka yamewasononesha wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda Waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano wao.
Madai ya kuonyeshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini hatukuweza kuamini hali itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu wanathubutu kudai na kuapa kuwa Hati hiyo haipo.
Ukweli ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote.
Hata hivyo, lazima tukubaliane kuwa zipo Hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho.
Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.
Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazifungua ili kuzihifadhi kwa namna yoyote ile. Lakini sasa maneno yanakua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.
Hivyo, kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli.
Hati hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi. Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.
Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi aione.
Mwisho, narejea kusema kuwa kwa upande wa Serikali tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba labda waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo Watanzania wenzetu, wafikie hapo. Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi waliosaini waasisi wetu.
Matumaini yetu ni kuwa baada ya leo tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa kisheria.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu,
DAR ES SALAAM.
14 Aprili, 2014
0 comments:
Post a Comment