Wednesday, March 26, 2014

MRADI WA TIER 1 KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bw Edward Sungura( Kaunda Nyeusi) akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Bw Julian Raphael, vifaa mbali mbali vya utekelezaji wa mradi wa TIER 1 mjini Zanzibar.
Mazingira ya biashara nchini yataendelea kuimarika na kuinufaisha nchi na wananchi kwa ujumla iwapo mradi wa Tier 1 utatekelezwa kikamilifu kwa wakati na kwa kuzingatia malengo yanayokusudiwa.

Mradi wa TIER 1 ni mradi unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP wenye lengo la la kujenga uwezo wa kuchambua, kushirikisha kuongeza ufanisi wa watendaji wa Serikali katika Sekta ya Viwanda, Biashara na Masoko ili waweze kuboresha Sekta hiyo na kuifanya kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi.

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa vya utendaji kazi kwa wa Watendaji wa Mradi wa TIER 1 ofisi ya Zanzibar, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania Bw Edward Sungura amesema, Serikali itaendelea kuboresha sekta za VViwanda, Biashara na Masoko kwa lengo la kuinua pato la nchi na wananchi wake wanaoendesha maisha yao kwa kutegemea sekta hizo.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na gari moja na vifaa vya ofisi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mia moja za Kitanzania.
Akipokea vifaa hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar Bw Julian Raphael amesema, Ushirikiano wa Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar unatoa nafasi ya kukua kwa sekta hizo na kushawishi wafadhili kusaidia kwa rasimali fedha na vifaa ili kufanikisha mipango mizuri iliyopo.

Bw Raphael ameongeza kuwa, vifaa vilivyotolewa vitatunzwa na kutumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa. Aidha, katika hafla hiyo, Mratibu wa Mradi wa TIER1 Bw Stevenson Ngoda alitambulishwa rasmi kuchukua jukumu la kuongoza shughuli za mradi huo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU),
Wizara ya Viwanda na Biashara,
DAR ES SALAAM.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI