Tuesday, October 6, 2015

UVCCM WAMJIBU KINGUNGE, WASEMA KAKOSA UUNGWANA

Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya CCM (UVCCM) imesema uamuzi wa aliyekuwa kada wa chama hicho, Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kukihama chama hicho ni ukosefu wa uungwana katika dhana ya siasa pamoja na uimla usiokubalika katika siasa za kileo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Shaka Hamdu alisema licha ya Kingunge kukulia ndani ya umoja huo na kushika nyadhifa mbalimbali ameshindwa kuheshimu matokeo ya mchuano wa nguvu ya hoja na kutaka kulazimisha fikra zionekane sahihi.

Shaka alisema umoja huo unamshangaa Mzee kingunge ambaye amekuwa mwanachama wa jumuiya hiyo hadi kufikia kuwa Katibu Mkuu wa Pafmeca Youth kuibuka na kukiponda chama alichokitetea katika uhai na maisha yake yote na kuapa kuwa hakitatokea chama bora nchini kitakacholingana na CCM.

“Tokea akiwa kijana mdogo, Mzee Kingunge amekuwa mwanachama wa jumuiya yetu hadi kufikia kuwa Katibu wa Pafmeca Youth iliyokuwa na makao yake makuu nchini Algeria…. lakini amekosa uungwana katika dhana ya siasa, alichofanya ni uimla na ufashishti usiokubalika katika siasa za kileo” alisema Shaka.

Alisema tangu awali kada huyo wa zamani wa CCM alikataa kusimamia taratibu za kumsaka na kumpata mgombea urais kulingana na sifa na badala yake akamtaka mgombea aliyepungukiwa na sifa na vigezo.

Aliongeza kuwa, Kingunge alishindwa kukubali ukweli kuwa urais ni taasisi adhimu yenye staha na kujikita kumpigania mgombea mmoja ambaye hakuwa na sifa zinazolingana na hadhi ya chama hicho.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI