Wednesday, September 16, 2015

ZITTO KABWE: CCM IMEOZA.....HAIWEZI KUBADILIKA HATA AKIJA MALAIKA KUIONGOZA


KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) hata kipate malaika hakiwezi kubadilika, hivyo dawa pekee ni kukiondoa jumla madarakani.

Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kituo cha basi Tabata Segerea, Zitto alisema matatizo mengi ya nchi yamesababishwa na sera mbovu za CCM ambazo baadhi ya wagombea wake ndio waliokuwa wakizitunga, kuzitetea na kuzitekeleza.

Kuna ambao wamekuwa watawala tangu tupate uhuru na bado wanataka waendelee kutawala, ukiwauliza wanasema tupeni tena kipindi kingine.

Sisi tunataka wote waondoke, tunataka tuweke mwanzo mpya katika nchi hii ndio maana hata ilani yetu imejikita kutatua changamoto mbalimbali zinazotukabili,” alisema Kabwe.

Zitto aliyewasili viwanjani hapo saa 10:14 jioni na kuanza kuhutubia saa 11:13 jioni, alisema taifa linakabiliwa na changamoto kuu nne ambazo ni umaskini, huduma mbovu za jamii, kukosekana kwa umoja wa kitaifa na ufisadi.

Leo hii tumekua na uchumi ambao hauzalishi ajira na kusababisha vijana wengi wanaomaliza masomo yao kuhangaika kutafuta kazi. Ni kwanini uchumi ambao unakua kwa kasi hauzalishi ajira,?” alihoji Kabwe.

Alisema hivi sasa nchi imekuwa na matabaka kwenye huduma za jamii kama vile elimu na afya na kusababisha Taifa kuwa la masikini na matajiri.

Leo hii watoto wa masikini na matajiri hawakutani, wa matajiri wanasoma shule zao halikadhalika na wa masikini…matajiri wanafundishwa elimu bora wanaandaliwa kuja kuwatawala masikini.

“Rushwa kubwa ndio inalitafuna taifa hili, mwaka jana zilitengwa Sh bilioni 546 kwa ajili ya kununulia madawa muhimu lakini ni Sh bilioni 36 tu ndizo zimetolewa, kuna wajanja wachache wamezifanyia ufisadi zile fedha,” alisema.

Kiongozi huyo wa ACT, alisema wamejipanga vizuri na wamesimamisha wagombea ubunge 219 nchi nzima hivyo akawataka Watanzania kuwapima kulingana na uwezo wao kisha kufanya uamuzi.

Awali mgombea ubunge katika Jimbo la Segerea, Mohamed Mwikongi, alisema akifanikiwa kushinda kiti hicho ataanzisha mfuko wa maendeleo wa Segerea na kuwahamasisha wananchi wajiunge katika vikundi ili wapate mikopo.

Nitaangalia upya mfumo wa wazazi kuchangia gharama za elimu katika shule za umma na kuzipunguza ili ziendane na hali halisi ya utendaji,” alisema Mwikongi.

Naye mjumbe wa chama hicho, Terry Gbemundu, alisema Watanzania wengi wameaminishwa kuwa ni masikini lakini hakuna umasikini wowote nchini.

“Tunaaminishwa hivyo ili tuibiwe tuzidi kukandamizwa, akili zimedumazwa lakini sasa uamuzi mnao kwenye sanduku la kura.

Atakayechagua kijani (akimaanisha CCM) ambayo imetawala kwa miaka 54 bila mafanikio sijui itabidi tukapimwe akili,” alisema Gbemundu.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI