Wednesday, September 16, 2015

LOWASSA - "OLE WAO " SOMA HAPA ALICHOSEMA!!!

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amewaonya viongozi watakaowanyanyasa wamachinga, mama ntilie na waendesha bodaboda baada ya yeye kuingia madarakani.
Amesema pamoja na kwamba Serikali yake itamjali kila Mtanzania, makundi hayo matatu ni marafiki zake na anajua umuhimu wao katika kukuza uchumi wa taifa.
Kutokana na hali hiyo, amesema hatasita kumchukulia hatua kiongozi yeyote wa Serikali atakayeyanyanyasa makundi hayo kwa kuwa ni marafiki zake.
Lowassa ambaye anaungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitoa onyo hilo mjini Kahama jana alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni katika uwanja wa stendi mpya uitwao Mbulu.
“Matumaini ni makubwa sana mwaka huu, naomba Mungu anisaidie kwa sababu nakubaliana na mgombea ubunge wenu, James Lembeli, kwamba Kahama unatakiwa kuwa mkoa.
“Nasikitika pia ile bandari kavu ya Isaka kutofanya kazi, lakini nikifanikiwa kuingia madarakani, nitalifanyia kazi hili.
“Nasikitika vilevile kusikia habari ya maji, kwamba kuna maeneo hapa Kahama hamna maji, nawaahidi nikiingia madarakani, nitalimaliza hili na maji mtapata.
“Lakini, ole wao watakaowanyanyasa mama ntilie, wamachinga na waendesha bodaboda. Watu hawa ni marafiki zangu na nitakapoingia madarakani, nitawaboreshea maisha yao ikiwa ni pamoja na kuwaanzishia benki yao.
“Nawaahidi pia kufuatilia suala la operesheni tokomeza ili walioathiriwa walipwe fidia na jambo hili nililisema pia wakati nikiwa Katavi na Rukwa,” alisema Lowassa.
Aidha Lowassa alisema pamoja na kwamba kuna watu wanadharau uamuzi wake wa kuomba urais, lakini amelazimika kuomba nafasi hiyo kwa sababu amechoshwa na umasikini walionao Watanzania.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania wawe makini siku ya kupiga kura ili wamchague yeye na wagombea wa Ukawa kwa sababu wanachukizwa na umasikini wa Watanzania.
“Nimekuja hapa Kahama kuwaomba kura kwa sababu kura zenu ni muhimu sana kwangu. Hamjui ni kwa kiasi gani mnavyogusa moyo wangu pindi ninapoona maelfu ya watu mnakuja kwenye mikutano yangu kama hivi na mnanishangilia.
“Nawaambieni mnanipa imani nami nawaahidi utumishi uliotukuka, nawaahidi kwa sababu imani huzaa imani.
“Nimegombea urais kwa sababu nimechoshwa na ulegelege wa Serikali, nimegombea urais kwa sababu nataka kuunda Serikali yenye spidi kali ambayo haijawahi kutokea na itakayowajali wakulima, wafugaji, wachimbaji wadogo wadogo na Watanzania wote kwa ujumla.
“Nawaambieni kabisa, kwamba nataka nchi yangu ipae kimaendeleo, biashara ndogondogo zote zitafanywa na wazawa, biashara kubwa kubwa wazawa watakuwa na asilimia 70 na wageni watakuwa na asilimia 30, na nataka pia kila aliyekuwa akila mlo mmoja, ale milo miwili, aliyekuwa na baiskeli moja, awe nazo tano na aliyekuwa na ng’ombe kumi awe na ng’ombe 20.
“Siku hiyo ya Oktoba 25 mwaka huu ni siku muhimu sana kwetu, fikirieni nani wa kupigia kura, fikirieni mara mbilimbili kwa sababu siku hiyo ndiyo siku ya kuwaondoa CCM madarakani,” alisema.

Chanzo-Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI