Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameushutumu utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kukumbwa na kashfa nyingi ikiwamo ya usafirishaji wa meno ya tembo huku wahusika wakifichwa.
Akiwahutubia wananchi wa Manyoni, mkoani Singida, katika kampeni za mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, alisema inashangaza Serikali ya CCM ikiwaacha wananchi wake wanateseka kwa kukosa huduma muhimu huku watu wachache wakisafirisha nyara za serikali.
Aliwaomba wananchi hao kuiondoa serikali ya CCM madarakani kwa kumchagua Lowassa ambaye anaungwa mkono pia na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ili awaundie serikali inayowajibika.
“Inashangaza kipindi chote cha utawala wa CCM kumekuwa na kashfa nyingi ikiwamo ya kukamatwa kwa pembe za ndovu lakini wanaokamatwa na nyara hizo za serikali hawatajwi,” alisema.
Sumaye alisema CCM imekumbwa na kashfa za Tegeta Escrow, iliyohusu uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 zilizokuwa zimehifadhiwa Benki Kuu (BoT) kutokana na mgogoro wa malipo Tanesco na IPTL.
Uagizaji mafuta nje, mradi wa dhahabu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania Meremeta, Richmond na uagizaji mabehewa mabovu ya Kampuni ya Reli (TRL).
Alitaja usafirishaji wa twiga hai kwenda ughaibuni, kunaswa mara kadhaa meno ya tembo yakitokea bandari ya Dar es Salaam na mengine yakipitia kwenye uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.
Aliongeza kuwa serikali ya Lowassa haitaagiza mabehewa mabovu, haitaagiza meli na vivuko vibovu na kutengeneza barabara mbovu, haitawaacha wananchi wateseke kwa kukosa dawa hospitalini bali itafanya mambo mazuri yatakayowafanya wananchi wasonge mbele kimaendeleo.
“Watu wenye akili ndogo kazi yao huishia kuzungumzia watu,watu wenye akili ya kawaida huzungumzia matukio,na watu wenye akili kubwa huzungumzia mipango ya mbele ndio akina Lowassa,” alisema.
Alisema hospitali zinakosa dawa, akina mama wakienda kujifungua wanaambiwa waende na vifaa na hiyo inatokana na utapeli unaofanywa na Serikali ya CCM.
Sumaye alisema Lowassa akichaguliwa ataunda serikali inayowajibika kwa wananchi na siyo inayojali matumbo yao na kuwataka wananchi wasitishwe kuchagua upinzani.
Aliwaambia wananchi hao kuwa yeye na Lowassa walijiondoa CCM baada ya kuona chama hicho hakiwezi kuwaletea maendeleo wananchi.
Alidai kuwa kutokana na CCM kuwa na hofu ya kushindwa kwenye uchaguzi , baadhi ya watendaji wameanza kupita na kukusanya vitambulisho vya kupigia kura kwa madai wanavisajili ili baadaye kutoa msaada wa chakula na kuwataka wananchi wasikubali kutoa shahada zao.
“Safari hii hawaibi kura, tutawadhibiti, tutalinda, hakuna mtu anayeweza kushinda na nguvu ya umma,” alisema.
Kwa upande wake mgombea ubunge jimbo la Manyoni, Emmanuel Mpandagoya, alimweleza Lowassa kwamba akichaguliwa kuwa rais asaidie kulipatia ufumbuzi tatizo la maji ambalo limekuwa sugu katika jimbo hilo.
Kwa upande wake Lowassa amesema akiingia Ikulu atahakikisha anaunda serikali itakayofanyakazi kwa mchakamchaka itakayoleta maendeleo kwa wananchi na kuonya asiyeweza kasi hiyo ajitoe mapema.
Lowassa ambaye hadi sasa amefanya ziara katika baadhi ya majimbo ya mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi, Kigoma,Tabora, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Sindida, alisema kwa miaka 50 sasa serikali ya CCM imeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi hivyo wasiharibu kura yao kwa kuendelea kuichagua CCM.
Alisema kama wananchi watamchagua tatizo la maji linaloukabili mji wa Manyoni itakuwa historia na kwamba ni jambo la kushangaza toka Tanzania imepata uhuru hakuna maji na wananchi wamekuwa wakiahidiwa maisha bora.
“Mna maji hapa…hakuna, mna afya bora…hakuna, mna kilimo bora..hakuna, sasa pigeni kura vizuri ili niwaletee maendeleo kwani mabadiliko ya kweli hayawezi kupatikana ndani ya CCM isipokuwa Ukawa,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.
Alisema Watanzania wamechoshwa na umaskini na hivyo kuwataka kujitokeza kupiga kura na kuhakikisha wanazilinda ili zisiweze kuibiwa.
AFURAHIA BANGO
Lowassa alikatisha hotuba yake na kuamua kusoma bango lililokuwa limeandikwa na vijana linalosomeaka ‘Mnashangaa Lowassa kupanda daladala hamshangai Twiga kupanda ndege”.
LISSU
Mwanasheria Mkuu wa Chadema,Tundu Lissu, alisema Lowassa na Sumaye wana maisha mazuri lakini wamekubali kujiunga upinzani ili kuivusha nchi kimaendeleo katika kichaka cha CCM.
Alisema mawaziri wakuu hao wangeweza kuendelea kula raha kwasababu hadi sasa bado wanaendelea kulipwa asilimia 80 ya mshahara lakini wameamua nchi hii isipoondoswa CCM itakuwa tabu.
#NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment