Monday, September 21, 2015

LOWASSA KUSAFISHA MASHANGINGI...ELIMU BURE!!!

MGOMBEA urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amewatoa hofu wananchi kuhusiana na ahadi yake ya kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi Chuo Kikuu kwa kueleza kuwa fedha zipo za kutosha zikiwamo zitakazookolewa kutoka kwenye magari tele ya kifahari aina ya Land Cruiser 'mashangingi' yanayotumiwa kila uchao na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza mbele ya umati Chanika katika Jimbo la Ukonga, Wilaya ya Ilala na baadaye kwenye Jimbo la Mbagala jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema kipaumbele chake cha kwanza ni elimu aliyosisitiza kuwa itatolewa bure kwa kila mtoto na kwa kila ngazi hadi chuo kikuu.

Kadhalika, Lowassa alisema ameamua kugombea urais kwa sababu anaweza, ana utashi na amepania kupambana na umaskini unaowakabili Watanzania kwa muda mrefu.

Akizungumzia sekta ya kilimo, Lowassa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Rais Kikwete, alisema akichaguliwa wakulima hawatatozwa ushuru wa mazao yao.

Aliahidi pia kufanya mabadiliko makubwa katika serikali atakayoiunda ili ifanye kazi kwa spidi kubwa, huku akieleza vile vile kuwa serikali yake itatoa mazingira mazuri ya kazi kwa waendesha bodaboda, mama lishe na Wamachinga ili wajikwamue kiuchumi na siyo kuwabughudhi kama inavyofanyika sasa.

Aidha, Lowassa aliahidi kuanzisha wizara maalum itakayoshughulikia uendeshaji makini wa Jiji la Dar es Salaam na kuwaondolea wananchi wake kero mbalimbali zilizopo.

Awali, Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji, aliitaka CCM ijiweke tayari kuondoka kwani Ukawa itashinda na kuingia Ikulu.


Mwenyekiti wa Chadema , Freeman Mbowe, amtaka Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva, kuionya CCM kutokana na matamshi anayotoa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM , Abdallah Bulembo, kwamba chama chake hakitaachia Ikulu hata kama kitashindwa uchaguzi.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, alisema haipendezi kwa mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli, kutumia nembo ya M4C (Movement for Change) ambayo ni mali ya Chadema na kujinadi nayo kwamba ni 'Magufuli for Change'.

Mwishoni mwa mkutano katika eneo la Mbagala Zakheem, maelfu ya wananchi walisindikiza msafara wa Lowassa na shughuli za biashara maeneo ya jirani kusitishwa kwa muda.

#NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI