




Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Kituo cha Utamaduni cha Ujeruman maarufu kama Goeth Insitut wameendesha mafunzo ya utengenezaji batiki kwa wasanii wa Sanaa za mikono yanayofanyika kwenye Ukumbi wa BASATA jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yanayotazamiwa kudumu kwa siku tano yaani kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa yanalenga kuongeza ubunifu na weledi miongoni mwa wasanii wa Sanaa za mikono ili kuongeza ubora na tija katika uzalishaji.
Mapema akizungumza kwenye uzinduzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Utamaduni chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Leah Ruhimbi alisema kwamba mafunzo hayo yatasaidia kuongeza tija kwa wasanii hao na kuwawezesha kubuni Sanaa zenye ubora zitakazopenya masoko mbalimbali ya Sanaa.
“Ni matarajio ya BASATA na wizara kwamba mafunzo haya yatakuwa yenye tija kwa wasanii na yatawawezesha kusambaza ubunifu na uzoefu kwa wasanii wengine nchini. Lengo ni kuwa na sanaa zenye ubunifu na ubora” alisisitiza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Goeth Institut Bi. Eleonore Sylla alisema kwamba mafunzo hayo yanahusisha wasanii wenye uwezo wa kutengeneza batiki na lengo kuu ni kuwaweka pamoja ili wachangie uzoefu na baadaye kutengeneza batiki zenye ubora zaidi.
“Tunajua mnatoka sehemu mbalimbali nchini na wote mna uzoefu katika utengenezaji wa batiki lakini kuwa kwenu pamoja kwenye mafunzo haya kutawafanya mpate uzoefu zaidi na hatimaye kubuni batiki zenye ubora” aliongeza Sylla.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza alisema kwamba BASATA kwa kushirikiana na Goeth Insitut wameona kwamba kuna haja ya mafunzo hayo ya wasanii na kwamba baraza litaendelea kuboresha ubora wa kazi za Wasanii kupitia kuwajengea uwezo.
Picha, habari na Aristide Kwizela-Afisa Habari BASATA
0 comments:
Post a Comment