Saturday, October 25, 2014

NI NANI ANAYECHANGIA KUVUNJA NDOA: MKE AU MUME?

Soma barua kali toka kwa mdau wa Diary yangu….!
LEO nimeamua kukuandikia jambo moja linaloninyima raha,…kama halitifaa kuliweka hewani nirudishie, na kama litafaa lipitie vyema, kama nimekosea Kiswahili nirekebishe maana tumeloea Ulaya hata lugha sasa inatupiga chenga. Kwa ujumla nimekuwa nikipitia mitandao mingi, na mingi imekuwa haielezi ukweli kuhusu mwanamke na mwanaume, hasa NDOA, Naizungumzia ndoa, kwani mimi nipo ndani ya ndoa, nana bahati ya kuishi kwetu bongo kwenye manyayaso ya hali ya juu ya ndugu na mama mkwe na pia kuja kuishi Ulaya, ambapo maisha yetu sio mabaya, tunakula ….Sasa ubaya upo wapi, najua wengi mtauliza, nakuwaza, Ubaya upo ndani ya ndoa yenyewe, ubaya upo kwenye kusikilizana, ubaya upo kwenye maisha ya mke na mume, mimi huku ni kama mfanyaakzi wa nyumbani, ninaweza kusema mimi ni mmoja wa wahanga wa ndoa,ingawaje nipo dunia ya sasa, ninaishi Ulaya na mume wangu, lakini maisha ninayoishi na mume wangu ni kama tupo ile dunia ya mababu zetu ambayo mke hana usemi.

Mke ni kama bidhaa, yote nimevumilia sikujali kuwa nipo Ulaya, na kama ningeliamua kufanya lolote ningeliweza, lakini bado naiheshimu ndoa yangu. Mimi hapa nipo kama mshumaa tu, siku yoyote unaweza ukazima, na ni bora niyasema haya ili watu wajifunze na waysikie, mwanga wa mshumaa huu usiishie kwangu tu, uwamulikie na wengine wanaoteseka kama mimi.
Najua wengi mtanilaumu kuwa natoa siri yangu ya ndoa, lakini nimeona ni heri kufanya hivyo, ili iwe chachu kwa wale wanaume wengine wenye tabia kama hizi waweze kubadilika, ila kwa mume wanu imeshindikana, imekuwa kama mbuzi kupigiwa gitaa. Hapa nilipo umri umeshapevuka, siwezi kusema niachane naye, nikatafute mume mwingine, nani atanioa mimi wakati sura imeshachujuka. Sitaweza kuwatelekeza watoto wangu kwa kuabdili wanaume, hapana, ila nahitaji mawazo yenu, ….Kwanini naandika haya : Nimeamua kuyaaandika kwasababu kuna mtu aliuliza swali, je kati ya wanandoa wawili mke na mume ni nani anayechania kuvunja ndoa. Ndio sisi wanawake tunakuwa na kitu kinachoitwa kitchen party, je inatusaidiaje kudumisha ndoa zetu, huyu mtu aliuliza hivyo, nikashindwa kumuelewa kwani ndoa ni watu wawili, kama mke atajitahidi sana na mume bado haelewi hiyo ndoa, au hayo mafunzo ya kitchen party yatasaidia nini.
Nimefikiri sana, na kufanyia utafiti ukianzia kwangu mwenyewe na kugundua kuwa kati ya mwanaume na mwanamke anayechangia kwa kiasi kikubwa kubomoa ndoa,ni mwanaume ila nchi za kwetu,hasa nchi za dunia ya tatu(maskini,afrika)wanamwangalia mwanamke kama ndiye chanzo cha kuvunjika ndoa, hasa wakisema, eti wanawake wengi haweze kumtuliza mume, hawajitahidi kumshawishi mume atulie nyumbani na ndio maana wanatafuta nyumba ndogo n.k swali hapa ina maana mke pekee ndiye anatakiwa kufanya jitihada hizo?
Hebu tuziangalie jitihada za mwanamke hasa wa Kiafrika, na tujiulize mwanamume anataka jitihadi gani zaidi ya hizo, kwani,mwanamke wa kiafrika,anamoyo ule wa kuvumilia,maudhi pamoja na manyanyaso ya kila aina,anayofanyiwa na mume wk.

Mfano,kupigwa, kuishi na mwanamume mlevi, kumvumilia mwanamume hata akichelewa kazini kwa visingizio mbali mbali,kuletewa watoto wa nje,au hata kuletewa nyumba ndogo au vimada nk.Lakini yote hayo,anayabeba ndani ya moyo wake,na anaona kuwa ni aibu ya ukoo,yeye kurudi kwao,kwa kisa,ameshindwa kuvumilia ndoa.Wanawake wengine,hadi wanapata vilema vya maisha,kwenye ndoa zao na bado wapo kwenye ndoa wanavumilia na kuendelea na maisha kama kawaida.Wengine,wanawafumania waume zao,lakini,wanabakia na siri na kuwatetea waume wao,kuwa hakufanya jambo lolote baya na vitu kama hivyo, je uvu,milivu gani kama huo, upendo gani kama huo, uvuto upi mnaoutaka, kucheza sebene peke yake.Hebu chukulia upande wa pili kwa mwanaume mfano mwanaume,akufumanie,itakuwaje, wewe uchelewe kurudi nyumbani itakuwaje, ….ukosee kufanya jambo fulani, na mengine mengi, mwanamke atakiona cha mtema kuni.
Kwa ujumla Ndoa,inaumiza sana kwa wanawake.Na vidonda vya ndoa au majeraha ya ndoa,ni mengi sana kwa mwanamke na hayaponyeki, kwani kila siku yanatoneshwa…Kwa ujumla mwanamke wa Kiafrika anastahili kupewa heko, na hili nimejifunza nilipokuja kuishi huku Ulaya. Huku Ulaya mwanamke ana haki zake, hayanyanyaswi ovyo,na ole wako mwanamume umnyanyase mkeo halafu alifikishe hilo swala kwenye vyombo vya sheria….sio kwamba nawasifia kwa hili, lakini kwa kiasi kikubwa limemkomboa mwanamke na kujiona kumbe na yeye ni kimumbe kama mwanaume.Mimi nimeishi maisha hayo ya taabu hata vile nipo Ulaya, nimekuwa nikiishi na mume wanu na kumfanyaia yote kama vile nipo nyumbani, lakini ….nasema lakini ni ule usemi usemao penye miti mingi hakuna wajenzi…imefikia mume wangu hawajabiki kwenye swala muhimu la ndoa yake, swala ambalo wengi wanatulaumu kuwa sisi sio wabunifu, hatujui mapenzi, lakini utajuaje kucheza mpira kama hujaingia uwanjani…hayo ni visingizio vyao na kusema ukweli kama hilo wao ndio wakulaumiwa, kwani walitakiwa kushirikiana na mkewe wakafundishana na kuelekezana sio kukimbilia vimada.
Uvumilivu una mwisho wake, na majeraha yakizidi sana mwisho wake yanaweza kugeuka kuwa kansa, ndio maana nimeandika hilo swala kwako, uliweke hadharani watu walijadili na wanaume wasema ukweli wao, ili sisi wanawake tujue ni nini hasa waanume wanakihitaji kutoka kwetu, ili tuwatimizie,… ili tukiwafanyia hivyo waweze kutulia majumbani kwao, ili mwisho wa siku ndoa ziwe na amani.Humutaamini kuwa wengine tunamaliza miezi zaidi ya mitatu hatuwajui waume zetu, waume zetu huku Ulaya wanasingizia kuwa wanachoka kwenye kubeba maboksi, je ni kweli hili au ni kisngizio cha mume wangu tu, au na wenzangu wanafanyiwa hivyo hivyo, …je huko wanaposhinda na hata kulala na machangudoa hawachoki, au wanatufanya sisi ni wajinga tu hatjui nini wanachokifanya, je hii ni ndoa kweli, je na sisi tukiamua kutoka nje ya ndoa waatsemaje, na kwa hilo ni nani atalaumiwa, lakini tunaogopa kuja kuwaacha watoto wetu mayatima kwa kuugua magonjwa mabaya. 
Samahani sana kama nitakuwa nimewakwaza wengine kwa hayo niliyoyaongea lakini kama ilivyo kawaida ukweli huuma, …
Mimi mwenye majeraha ya ndoa Mama Wawili.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI