Friday, May 30, 2014

SAFI SANA NKAMIA, KUNA HAJA GANI YA KUJIITA `SIMBA` WAKATI UWEZO WAKO NI KAMA `SUNGURA`

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
SERIKALI kupitia wizara ya habari, vijana, utamaduni na michezo inatarajia kuliagiza shirikisho la soka Tanzania kuachana na mpango wake wa kubadili jezi na jina la timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Naibu waziri wa wizara hiyo, Juma Suleiman Nkamia, mwanahabari kitaalum na mtangazaji wa zamani wa michezo TBC, amesema hakuna haja ya kubadili jina, kikubwa ni kuubadilisha mchezo wenyewe ili twende sambamba na dunia ya sasa.
Hata hivyo, Nkamia alisema serikali inaendelea na jitihada zake za kujenga na kuimarisha miundombinu ya michezo kulingana na uwezo wake.
Watu walisema mapema kuwa TFF kwasasa hawana haja ya kuhangaika kutafuta jina jipya kwa timu ya taifa hususani jina linalotisha kama ilivyo kwa nchi za Magharibi.
Ukisikia majina ya nchi kama Ivory Coast, Nigeria, Senegal, Morroco, Cameroon na nyinginezo, lazima uhofie kabla ya kukutana nazo.
Tembo wa Afrika (Ivory Coast) , Simba asiyefugika (Cameroon), Simba wa Teranga (Senegal), kweli ni majina yanayovutia na kuogopesha, lakini ukweli ni kwamba mataifa haya kweli yako vizuri kisoka.
Huo ndio ulikuwa mwonekano wa jezi ya Taifa stars kabla ya kubadilishwa siku za karibuni
Majina yao yanatisha na wanatisha kweli wakiingia uwanjani. Kwahiyo majina yao yanasadifu uwezo wao uwanjani.
Inapokuja kwa nchi kama Tanzania, kuna haja gani ya kuhangaika kutafuta jina la kutisha wakati timu yenyewe imedoda kwa miaka mingi.
Leo hii unaona Taifa Stars halifai, kwani ukitafuta jina linalotisha litakusaidia nini wakati wewe hutishi.
Kuna mambo mengi ya kufanya katika soka letu kwasasa na jukumu kubwa ni kutafuta mfumo mzuri wa soka la vijana na kuboresha miundo mbinu.
Tunategemea kwasasa viongozi wahangaike na ujenzi wa vituo vya michezo, vyuo vya michezo ili kulijenga soka la vijana kama walivyofanya Nigeria, Ivory Coast, Ghana na kwingineko.
Msingi wa mpira unajengwa katika soka la vijana na sio kuhangaika na vitu vidogo kama kubadilisha jina la Taifa stars na mipango kama maboresho ya Taifa Stars. Mipango ya muda mfupi haifai, njia za mkato kama hizi hazina maana kwasasa.
Serikali ipo sahihi inaposema hakuna haja kabisa ya kubadili jina na wadau wengi wanaamini hilo.
Kuna haja gani mtu kujiita Cristiano Ronaldo, Lionel Messi, wakati kiwango chake hakisadifu jina.
Watanzania tunapenda kujipachika majina ya watu maarufu, lakini hatufanyi jitihada za kutafuta kuelekeana na majina yenyewe.
Utashangaa mtu wanayemwita Ronaldo au Messi anavyojihangaisha na mambo ya `kipuuzi`. Hana jitihada yoyote wala haendani na jina lenyewe.
Kuna haja ya kuachana na utamaduni wa kupachikana au kujipachika majina makubwa ambayo hatuwezi kuyabeba.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI