Friday, May 30, 2014

AL-MERREIKH KUKINUKISHA ROBO FAINALI CECAFA NILE BASIN CUP LEO, MBEYA CITY KESHO HAPATOSHI

Kocha bora wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014, Juma Mwambusi (kulia)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
ROBO fainali ya michuano ya CECAFA Nile Basin Cup inayoendelea kushika kasi nchini Sudan inatarajia kuanza kuunguruma leo jioni mjini Khartoum kwa mechi mbili kupigwa katika uwanja wa Merreikh.
AFC Leopard waliomaliza wa kwanza katika kundi B kwa kukusanya pointi 9 (ushindi wa asilimia 100) watakabiliana na Defence ya Ethiopia majira ya saa 12:30 jioni kwa saa za Sudan.
Usiku saa 2:30, wenyeji Al-Merreikh walioshika nafasi ya kwanza kundi A Kwa kujikusanyia pointi 7 watakuwa na kibarua cha kufa mtu dhidi ya Academie Tchite ya Burundi.
Robo fainali za pili zitaendelea kesho jumamosi (Mei 31) ambapo mechi ya kwanza itakayoanza saa 11:30 jioni itakuwa baina ya wagonga nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc dhidi ya Victoria University ya Uganda.
Wawakilishi hao wa Tanzania walimaliza hatua ya makundi kwa kushika nafasi ya pili kundi B baada ya kujikusanyia pointi 4 katika michezo mitatu.
Mbeya City walianza kampeni zao kwa kuwafunga Academie Tchite mabao 3-2, mechi ya pili wakalala kwa mabao 2-1 dhidi ya AFC Leopard na mechi ya mwisho walitoka suluhu na Entincelles.
Ushindi katika mechi hiyo ni muhimu kwa kocha Juma Mwambusi kwani kucheza nusu fainali itakuwa historia nzuri ikizingatiwa ni mara yao ya kwanza kucheza michuano mikubwa ya kimataifa.
Hata kama walishiriki mapinduzi Cup mwanzoni mwa mwaka huu visiwani Zanzibar na kukutana na timu za nje ya nchi, michuano ya Nile Basin Cup inashirikisha timu nyingi za kigeni.
Kwa maana hiyo, Mbeya City wanahitaji ushindi ili kuwafurahisha watanzania wanaowaombea dua kila kukicha.
Mechi ya pili itaanza majira ya saa 2:00 usiku kwa kuwakutanisha Al-Shandi dhidi ya Malakia FC.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI