Boniface Wambura Mgoyo, Afisa habari na Mawasiliano, TFF |
SEMINA YA WAAMUZI YAANZA DAR
Semina ya siku mbili kwa waamuzi wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wale wa ngazi ya juu nchini (elite) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu inaanza kesho (Machi 15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Waamuzi na waamuzi wasaidizi 22 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki katika semina hiyo ambayo pia itahusisha mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test), na itamalizika keshokutwa (Machi 16 mwaka huu).
Baadhi ya waamuzi hao ni Charles Simon kutoka Dodoma, Dalila Jafari (Zanzibar), Ferdinand Chacha (Mwanza), Hamis Chang’walu (Dar es Salaam), Helen Mduma (Dar es Salaam), Israel Mujuni (Dar es Salaam), Issa Vuai (Zanzibar), Janeth Balama (Iringa) na Jesse Erasmo (Morogoro).
John Kanyenye (Mbeya), Jonesia Rukyaa (Bukoba), Josephat Bulali (Zanzibar), Lulu Mushi (Dar es Salaam), Martin Saanya (Morogoro), Mfaume Nassoro (Zanzibar), Mohamed Mkono (Tanga), Mwanahija Makame (Zanzibar), Ngaza Kinduli (Zanzibar), Ramadhan Ibada (Zanzibar) na Waziri Sheha (Zanzibar).
YANGA KUIVAA MTIBWA SUGAR VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Machi 15 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo mabingwa watetezi Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Nao vinara wa ligi hiyo, Azam wanaikaribisha Coastal Union ya Tanga katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kwa kuwakutanisha wenyeji Kagera Sugar dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.
WATANZANIA WATANO WATWAA UKAMISHNA CAF
Watanzania watano wameteuliwa kuingia kwenye jopo la makamishna watakaosimamia mechi mbalimbali za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwa mwaka 2014 hadi 2016.
Kwa mujibu wa orodha iliyotumwa na CAF kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Watanzania hao ni Alfred Kishongole Rwiza wa Mwanza na Hafidh Ali Tahir wa Zanzibar ambao wamerejeshwa tena kwenye jopo hilo.
Rwiza na Tahir ambao ni waamuzi wastaafu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na wakufunzi wa uamuzi walikuwepo kwenye jopo lililopita la 2012 hadi 2014.
Makamishna wapya kwa upande wa wanawake ni Elizabeth Mwanguku Kalinga wa Mbeya na Isabellah Hussein Kapera wa Dar es Salaam. Kamishna mwingine mpya kwa upande wa wanaume ni Muhsin Ali Rajab kutoka Zanzibar.
Wakati huo huo, CAF imeandaa semina kwa makamishna wanaume itakayofanyika jijini Cairo, Misri kuanzia Aprili 3 hadi 4 mwaka huu.
Watoa mada kwenye semina hiyo ya siku mbili ni Katibu Mkuu wa CAF, Hicham El Amrani, Mkurugenzi wa Mashindano wa CAF, Shereen Arafa na Naibu Mkurugenzi wa Mashindano wa CAF, Khaled Nassar.
Wengine ni Meneja wa Waamuzi wa CAF, Eddy Maillet, Mkurugenzi wa Habari wa CAF, Junior Binyam, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Mawasiliano wa CAF, Tarek el Deeb na Mkurugenzi wa Masoko na Televisheni wa CAF, Amr Shaheen.
Boniface Wambura Mgoyo
Media and Communications Officer
Tanzania Football Federation (TFF)
0 comments:
Post a Comment