MCHAKATO wa vituo vya redio na runinga kuwalipa wasanii kutokana na kupiga nyimbo zao umeanza kwa kusuasua baada ya Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota) kudai kati ya redio zaidi ya 100 na runinga zaidi ya 20 zilizopo nchini, ni vituo vitatu tu vikiwamo vya Mlimani tv, Azam tv na Joy Fm ya Kigoma ndivyo vilivyolipa mirabaha kwa kutumia kazi za wasanii nchini.
Mkaguzi wa Hakimiliki kutoka Chama cha Hakimiliki Tanzania (Cosota), Paul Mabula, alisema kutokana na kukumbwa na changamoto nyingi ikiwamo kufukuzwa na baadhi ya wamiliki wanapokwenda kuwataka walipe mirabaha hiyo, wamelazimika kuwaandikia TCRA ili wajue cha kufanya zaidi.
“Tumeiandikia TCRA ili itusaidie katika changamoto tunazokumbana nazo wakati wa kudai mirabaha kwenye vituo vya redio na runinga, baa na maeneo mengine mengi,” alisema Mabula.
Mabula aliongeza kwamba Cosota inakabiliwa na idadi ndogo ya maofisa ambapo kwa sasa ina maofisa sita na inawawia vigumu katika mapambano ya kazi za ukusanyaji wa fedha za mirabaha inayofanyika nchi nzima.
“Vipo vituo vilivyotaka tuvipeleke wanavyodaiwa lakini licha ya kufanya hivyo, hakuna vituo vilivyolipa zaidi ya hivyo vitatu,” alieleza Mabula jana kwenye ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) Ilala jijini hapa.
Hata hivyo, licha ya kusikitishwa na hali hiyo, baadhi ya wasanii na viongozi wa mabaraza ya wasanii nchini wameitaka Cosota kushirikisha mabaraza ya wasanii ili watoe watu wao wasaidie shughuli za ukusanyaji mirabaha kwa ajili ya manufaa ya kazi zao.
#Mtanzania
0 comments:
Post a Comment