Makala: Na MUSA MATEJA
KILA mtu ana historia yake katika maisha! Joseph Michael ‘Jose Mara’ yeye kutokana na historia ya kimaisha aliyopitia, amesema mkewe Monica Michael Joseph ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mungu.
KWA NINI NI ZAWADI YA KIPEKEE?
“Nadiriki kusema kuwa mke wangu ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mungu kwa kuwa kuna vigezo mbalimbali yaani ukiachia mbali tabia ambayo ni silaha kubwa kwangu kutokana na kuendana kwa kila kitu, ila kuna jambo lingine kubwa lipo ambalo wengi hawalifahamu.
Siku ya ndoa yao
ANAZIDI KUFUNGUKA
“Kama hujagundua mke wangu anaitwa Monica Michael Joseph, mimi naitwa Joseph Michael, hadi hapo utaona ubini wa majina yetu unaendana jambo ambalo linakuwa ni adimu sana kwa wanandoa wengi kuoana na mkakuta majina yenu ya pili yanafanana.
ILIKUWAJE?
“Kufanana kwa majina haya naweza kusema ndiyo zawadi pekee niliyopewa na Mungu, ndiyo maana leo hii tunaenda kutimiza miaka tisa ndani ya ndoa yetu ambayo ilikuwa ikibezwa sana na baadhi ya watu kufuatia wengi kuamini kwamba wanamuziki walio wengi huwa hawawezi kuishi na mke mmoja.
“Kabla sijamuoa mke wangu nilibahatika kuishi naye zaidi ya mwaka huko nyuma kwani ndoa rasmi nilifunga mwaka 2007, namshukuru Mungu hadi sasa tayari nina familia ya watoto wawili.
Jose Mara na mkewe Monica.
MTOTO NAYE AFUATA MAJINA YA UBINI
“Mwanangu wa kwanza anaitwa Michael Joseph, mdogo wake anaitwa Joseph Junior. Niliamua huyu mdogo kumpa jina hili kutokana na kuona upeo wake unaendana na mimi.
NDOA NI NGUMU?
“Kwenye maisha hakuna jambo rahisi hata siku moja zaidi kinachotakiwa kwa kila mtu ni kukaza kadiri uwezavyo ili utimize malengo, hakuna maisha yenye changamoto kama maisha ya ndoa hivyo ninachoweza kuwaambia wote ambao wamekuwa wakifikiria ndoa za wanamuziki hazidumu si kweli kwani kila jambo linataka uvumilivu mkubwa.
ATOA SOMO KWA WASANII
“Napenda kutoa wito kwa wasanii wenzangu wote, wanapotarajia kuingia kwenye maisha ya ndoa basi wawe wanahakikisha wanaingia kwa dhamira zote, wasanii tumejenga picha mbaya kwa jamii kuwa hatutulii.
Jose Mara ni msanii aliyeanza kuwika kwa uimbaji akiwa shule ya msingi, baadaye kutunga wimbo wake wa kwanza aliouita Wema wa Jirani, hapa alikuwa katika Kundi la Wasi Music Band.
MSIKIE
“Wimbo wangu huu wa Wema wa Jirani ulikuwa mzuri sana sema haukupata nguvu ya kutamba kwa kuwa enzi hizo bendi zilikuwa chache mno ukilinganisha na sasa, lakini tatizo lingine kubwa lilikuwa kwa upande wa vyombo vya habari navyo vilikuwa vichache hivyo namna ya kusambaza na wimbo kupigwa ilikuwa ni shida mno na bendi pia ilikuwa changa.
AMEPITA BENDI KIBAO
Jose Mara amepita kwenye bendi nyingi ndogondogo japokuwa alikita nanga kwa muda mrefu katika bendi ya FM Academia ambapo alifanikiwa kudumu zaidi ya miaka tisa.
Akiwa ndani ya bendi hiyo aliweza kushiriki kwenye nyimbo kibao ikiwemo Dunia Kigeugeu, Heshima kwa Mwanamke, Hana, Dotnata, Mpenzi na nyingine kibao, mbali na kushiriki kikamilifu katika bendi hiyo kabla hajatoka na kwenda kuanzisha Kundi la Mapacha Wanne ambalo baadaye lilisambaratika na kuwa Mapacha Watatu, alitunga wimbo uitwao Chozi la Yatima.
AUZUNGUMZIA CHOZI LA YATIMA
“Chozi la Yatima huo ndiyo wimbo pekee ambao ninaupenda katika tungo zangu karibu zote.”
KWA SASA…
Hadi sasa Jose Mara yupo kwenye Kundi la Mapacha Watatu ambao juzikati waliungana kwa mara nyingine tena na kuwa Mapacha Wanne, ambao ni Chaz Baba, Kalala Junior na Khalid Chokoraa.
MALENGO YAKE
“Mwaka huu natarajia kuachia nyimbo mbili mfululizo ambazo tayari nimeshaanza maandalizi yake katika Studio za Combination Sound. Kati ya nyimbo hizo, mmoja nimeupatia jina la Chozi la Mwanaume na mwingine Mapacha wa Sasa. Nyimbo hizi nitazifanya ndani ya bendi ya Mapacha Wanne
#GPL
0 comments:
Post a Comment