Siku moja baada ya
Rais Jakaya Kikwete kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
amtaje mhusika wa Richmond anayezunguka naye kwenye kampeni, Mbunge huyo
wa Singida Mashariki ameibuka na kudai kuwa Rais huyo ndiye mhusika kwa
kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kuteua na kuwawajibisha mawaziri.
Juzi,
akiwa Kigoma, Rais Kikwete alieleza kumshangaa Lissu kumtaka amtaje
mhusika wa Richmond wakati mtu huyo anazunguka naye kwenye mikutano ya
kampeni na kumtaka amtaje la sivyo yeye (Rais), atamtaja.
Akihutubia mkutano wa kumnadi mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa, mwanasheria hiyo alianza kwa kusema: “Sasa ndugu zangu naomba leo nimjibu Kikwete na tumalizane na hii habari ya Richmond."
Alisema mkuu huyo wa nchi ndiye mhusika kutokana na mamlaka yake na; “si
ya huyu Lowassa anayedai natembea naye kwenye kampeni. Hapa kwenye
mkono wangu nina taarifa ya mwaka 2008 ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume
ya Richmond, Dk Harrison Mwakyembe, sasa ni miaka zaidi ya saba tangu
isomwe bungeni.”
Lissu
aliyekuwa akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo
katika viwanja vya shule ya kiwanja cha ndege, alinukuu maelezo ya
taarifa ya Mwakyembe kifungu kwa kifungu na kueleza namna ambavyo
taarifa hiyo haikuweza kumtia hatiani Lowasa, bali aliwajibika kutokana
na makosa ya watendaji wake.
Baada
ya kueleza kwa kina taarifa hiyo, Mwanasheria huyo alisema Rais Kikwete
ndiye pekee mwenye mamlaka ya kuwateua mawaziri, akisema alimteua Nazir
Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha na ndiye mwenye mamlaka ya
kuwawajibisha.
Karamagi na Dk
Msabaha walikuwa wameshika uwaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati
tofauti wakati wa sakata la Richmond na walijiuzulu pamoja na Lowassa.
“Waziri
mkuu Lowassa baada ya kutokea kwa sakata hilo alimwendea Rais Kikwete
na kumweleza kuwa ‘kimenuka’ tuvunje mkataba baada ya wabunge wa
upinzani kuchachamaa kuhusu sakata hilo, lakini alikataa na kumweleza
kuwa hizo kelele za wapinzani zitaisha tu,”alisema.
Alisema
baada ya Lowassa kujiuzulu mwaka 2008, tayari mashine za kutengeneza
umeme zilishafika nchini na baada ya kujiuzulu haikufahamika
zilikokwenda na kwamba baadaye mkataba wa Richmond ukahamishiwa kwa
kampuni ya Dowans ambayo iliendelea kulipwa mabilioni ya shilingi.
Alimtaka
Rais Kiwete awaambie Watanzania kwa nini Serikali yake iliendelea
kuilipa Dowans mabilioni ambayo ilikuwa ya mfukoni na kwamba kama
Lowassa alifanya makosa kwa nini hajapelekwa mahakamani kwa miaka minane
tangu ajiuzulu.
“Rais
Kikwete asitake kumaliza hizi siku chache za kampeni zilizobaki kwa
shari na mimi na naomba niwaambie, Lowassa amefanya kazi katika umri
wake wote wa miaka 62 ndani ya CCM na Serikali yake, lakini ameamua
kuhamia huku kwa ajili ya kuleta mabadiliko na kuacha marupurupu yake
yote,” alisema Lissu.
Msikilize Tundu Lissu Akiongea Hapo Chini.
0 comments:
Post a Comment