Saturday, August 1, 2015

MSHINDI WA NAFASI YA UBUNGE VITI MAALUM CCM MKOA WA SINGIDA, AMPONGEZA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI, DK.KONE

IMG_1615
Mshindi wa kwanza wa nafasi ya ubunge viti maalum CCM mkoa wa Singida, Aysharose Ndogholi Mattembe, akiwashukuru wapiga kura 318 (hawapo kwenye picha). Aysharose  ambaye ni Mkurugenzi wa shule ya British Zanzibar ya Kisauni Zanzibar, alipata ushindi huo mnono baada ya kuwabwaga wapinzani wake 13 kwenye uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini hapa.
IMG_1574
Mshindi wa kwanza wa nafasi ya ubunge viti maalum CCM mkoa wa Singida, Aysharose Ndogholi Mattembe (kulia) akiwa na msindi wa pili ( kura 235)  nafasi ya ubunge viti maalum CCM mkoa wa Singida, Martha Moses Mlata (kushoto), kwa pamoja wakiwashukuru wapiga kura wao, muda mfupi baada ya kutangazwa washindi. Kwa nyuma yao,ni aliyekuwa msimamizi uchaguzi wa UWT mkoa ambao ulichagua wana CCM wawili nafasi ya ubunge viti maalum, Dk. Parseko Kone.
IMG_1618
Msindi wa kwanza wa nafasi ya ubunge viti maalum CCM mkoa wa Singida, Aysharose Ndogholi Mattembe (wa kwanza kushoto), akiwa na wapinzani wake 12 wakifuatilia ufungaji wa mkutano huo uliofanywa na Katibu UWT mkoa wa Singida, Angela Mirembe.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu, Singida
MSHINDI wa kwanza ubunge viti maalum (CCM) mkoa wa Singida,Aysharose Ndogholi Mattembe, amemshukru na kumpongeza msimamizi wa mkutano mkuu wa uchaguzi UWT uliofanyika hivi karibuni, Dk.Parseko Kone,kwa madai kwamba alitenda haki kitendo kilichochangia mkutano umalizike kwa amani na utulivu mkubwa.
Uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini hapa,Mattembe alizoa kura 318 na kufuatiwa na Martha Moses Mlata aliyetetea nafasi yake kwa kupata kura 235.
Akifafanua, Mattembe ambaye ni Mkurugenzi shule ya British Zanzibar iliyopo Kisauni,alisema msimamizi huyo ambaye ni mkuu wa mkoa wa Singida,alitenda haki kuanzia mwanzo wa mkutano hadi mwisho.
“Nadhani katika kutaka pasiwepo na malalamiko,msimamizi Dk.Kone,alitutaka sisi wagombea wote tuwepo kwenye chumba cha kuhesabia kura.Uwepo wetu ndani ya chumba hicho,kuliondoka kabisa wazo la  wizi wa kura kwenye uchaguzi wetu”,alisema.
Alisema kuwa kwa ujumla msimamizi alikuwa ‘fair’ kabisa na ndio maana hata wagombea waliopata kura ambazo hazikutosha, kwanza walishukuru uchanguzi umefanyika kwa haki na uhuru na waliondoka ukumbi wakiwa na amani ya hali ya juu pamoja na mashabiki wao.
Katika hatua nyingine,Mattembe aliwaahidi wajumbe wa mkutano huo zaidi ya 940,kwamba hatawaangusha na wategemee ushirikiano na vitendo atavipa kipaumbele zaidi.
Kwa upande wake  msanii maarufu wa filamu na aliyekuwa Mlimbwende nambari moja nchini mwaka 2006, Wema Sepetu ametingisha kwenye kura za maoni kuwania nafasi mbili za ubunge Viti Maalum (Wanawake).
 Katika kinyang’anyiro hicho, Wema alipata kura 90 akiwa nyuma ya wagombea wakongwe watatu; Diana Chilolo aliyeshika nafasi ya tatu kwa kupata kura 182, Martha Mlata aliyeibuka wa pili kwa kura 235 na AyshaRose Matembe aliyekuwa wa kwanza kwa kuzoa kura 318.
 Kwa mujibu wa msimamizi wa uchaguzi huo, Dk Kone, walioshiriki wengine kwenye uchaguzi huo na matokeo yao kwenye mabano kuwa ni Sarah Mwambu (74), Martha Gwau (44), Rehema Madusa (24), Aziza Ntandu (5), Mary Marco (3), Sofia Joseph (2), Salome Mpondo (1), Leah Samike (1) na Elizabeth Lucas (0)
Aidha, msimamizi huyo alimtangaza Sarah Mkumbo kuwa mwakilishi wa kundi la Walemavu wakati Hawa Athman alichaguliwa kuwakilisha kundi la Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Akitoa shukrani zake kwa wajumbe, Wema alisema kuwa anawashukuru wajumbe kwa kuonesha imani kubwa kiasi hicho kwake japo ni mara yake ya kwanza kujitokeza na akawahakikishia kuwa huo ndio mwanzo tu wa safari yake.
Naye Chilolo, ambaye ametumikia nafasi ya ubunge Viti Maalum mkoa wa Singida kwa miaka 15 na sasa ndiye  Mwenyekiti wa UWT mkoa, aliwataka washindi wote kushirikiana kwa dhati ili CCM ipate ushindi kwenye Uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI