Saturday, January 3, 2015

ATANGAZA KUUZA FIGO KWA SH 90 MILION, MOROGORO

MKAZI wa Morogoro, Andrew Germanis Chimulimuli ametangaza kuingiza sokoni figo yake ambayo amesema anaiuza Sh90 milioni ili kukabiliana na ugumu wa maisha.
Chimulimuli aliyefunga safari kutoka Ifakara, Morogoro hadi jijini Dar es Salaam ili kufanya biashara hiyo alisema ameamua kutoa kiungo chake hicho muhimu kutokana na ugumu wa maisha unaomkabili.
“Nimeamua kujitolea nafsi yangu ili niisaidie familia yangu, kwa sababu mimi si kitu kama sina fedha, ndiyo maana nimejitolea kutoa figo yangu nipate fedha,” alisema Chimulimuli.
Chimulimuli alisema anataka kuiuza figo hiyo kwa gharama ya Sh90 milioni ingawa alikubali kufanya mazungumzo ya kupunguza bei pindi atakapopatikana mteja.
Takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaeleza kuwa kuna wagonjwa 470,000 nchini ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi kabisa na wanahitaji upandikizaji.
Ingawa uamuzi wa Chimulimuli unaweza kuwa msaada kwa Watanzania wenye mahitaji, lakini kimaadili ya afya na kisheria, jambo hilo linakatazwa kufanywa kiholela hadi pale linapofuata taratibu.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Figo Tanzania, Jaji Frederick Werema aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba anashangazwa na hatua za baadhi ya watu kuchukua uamuzi wa kuuza figo kwa ajili ya kujipatia fedha.
“Kutoa figo ni kosa la jinai, lakini siyo hivyo tu, kutoa figo ni lazima ufuate taratibu za kisheria na za kitabibu,” alisema Jaji Werema miezi kadhaa iliyopita.
Biashara ya figo
Aprili mwaka jana, gazeti hili lilifanya uchunguzi na kubaini kuwa wapo Watanzania wanaouza figo zao kiholela kwa ajili ya kujipatia fedha.
Gazeti hili liliwasiliana na vijana kadhaa ambao kwa nyakati tofauti walikubali kuwa wanauza figo zao na baadhi wakieleza kuwa tayari walishauza kwa gharama za kati ya Sh50 milioni hadi Sh80 milioni.
Chimulimuli alisema kutokana na ugumu wa maisha, kipato chake kimekuwa kigumu sana na hakiwezi kukidhi mahitaji ya familia.
“Mtu akikuona kwa nje anaweza kukuona kama upo sawa na una maisha mazuri lakini ukweli ni kuwa nina maisha magumu sana,” alisema. Kuhusu hatima yake kiafya, alisema yeye ni msafiri na hawezi kuishi milele na hivyo bora auze figo yake iwe msaada kwa wengine wenye mahitaji.
“Ni bora nifanye kitu cha halali kinachoigharimu afya yangu mwenyewe badala ya kuiba au kufanya uhalifu mwingine,” alisema Chimulimuli.
Uchangiaji wa figo
Daktari bingwa wa figo katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Linda Ezekiel alisema uchangiaji wa figo ni mchakato mrefu na si suala la fedha tu.
Dk Ezekiel alisema mchakato wa kuchangia figo ni mrefu kwani mchangiaji hutakiwa kuwa na kundi la damu linalofanana na mgonjwa.
Alisema vipimo vya afya hufanyika ambapo maradhi yanayoweza kuambukiza kama homa ya ini, magonjwa ya zinaa na Virusi vya Ukimwi, navyo huangaliwa kwa umakini mkubwa.
“Ni lazima tuhakikishe mtu ameridhia kabisa kufanya hivyo na katika hali hiyo ni lazima tumfanyie mtu ushauri wa kisaikolojia na afahamu hatua za utoaji huo sambamba na madhara anayoweza kuyapata,” alisema.
Kuhusu changamoto ya maradhi hayo Dk Ezekiel alisema kusafisha figo ‘dialysis’ ni gharama kubwa ambapo kwa tiba moja mgonjwa hutakiwa kulipa Sh300,000 na tiba hiyo hufanywa angalau mara tatu kwa wiki.
Hata hivyo Dk Ezekiel alisema kwa anayechangia figo na kubaki na moja hawezi kupata madhara kiafya kwani figo moja ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi zake.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI