MAANDAMANO nchini Mexico yaliyochagizwa na kupotea kwa wanafunzi 43 wa chuo yamesababisha uharibifu mkubwa baada ya waandamanaji kuvamia na kuzichoma moto ofisi za serikali zilizopo katika jimbo la Guerrero
Mapema Jumatano katika siku ya pili ya maandamano waandamanaji hao walielekeza hasira zao kwa maafisa wa serikali wakiwalaumu kutochukua hatua zozote mara baada ya wanafunzi 43 wa chuo cha ualimu kupotea.
Miongoni mwa waandamanaji hao ni wanafunzi 500 pamoja na walimu wenye msimamo mkali walivunja bunge la jimbo la Guerrero, kwa kuchoma moto maktaba na chumba ambacho watunga sheria hufanyia vikao.
Muda mchache baadae waandamanaji walichoma moto idara ya elimu katika ofisi ya ukaguzi sehemu ya mji mkuu wa jimbo la Chilpancingo ambapo vikosi vya zima moto vimefanya jitihada za kuuzima moto kwenye majengo hayo.
Maandamano hayo yametokea baada ya mamlaka mapema Ijumaa iliyopita kukiri kuwa genge la wauaji katika mji wa Guerrero limekiri kuhusika na mauaji ya wanafunzi hao 43.
Serikali ya Mexico imesema inashirikiana na wachunguzi wa kimataifa wa kushughulikia haki za binadamu ili kubaini kilichowasibu wanafunzi hao waliopotea.
0 comments:
Post a Comment