Saturday, November 15, 2014

MAUAJI YAZIDI KUTIKISA KITETO....WALIOPOTEZA UHAI WAFIKA *PICHA*

Mapigano baina ya wakulima na wafugaji Wilayani Kiteto mkoani Manyara, yameendelea tena, ambapo watu wengine wawili wamefariki dunia jana na kufanya idadi ya waliouawa kuwa saba.
Awali, Novemba 11, mkulima Hassan Kondeja mkazi wa Kitongoji cha Bwawani Kijiji cha Matui aliuawa kwa kukatwa shingo na wafugaji na ndipo yakatokea mauaji ya wakulima wawili na wafugaji wawili.
Akizungumza na mwandishi wetu, Kamanda wa polisi wa Mkoa Manyara, SACP Deusdedit Nsimeki alisema wakulima wawili wameuawa jana kwa kukatwa na mapanga na watu wanaodaiwa kuwa ni wafugaji wa jamii ya Kimasai.
Kamanda Nsimeki aliwataja wakulima hao waliouawa ni Juma Omary (65) na Nyanya Ngoroka (70) wote wakazi wa Kijiji cha Cheka Nao, kata ya Kiperesa iliyopo mpakani na wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
“Chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi uliotokea kati ya wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye shamba la wakulima hao na walipowakataza wakatumia silaha za moto na kuwakata mapanga wakafa papo hapo,” alisema Kamanda Nsimeki.
Alisema vifo hivyo vinatokana na kulipiza kisasi kati ya wafugaji na wakulima ambao chanzo chake ni migogoro ya ardhi ya muda mrefu.
Naye, mkuu wa mkoa huo, Elaston Mbwilo alisema wapo baadhi ya viongozi wamekuwa wazembe hawawajibiki katika nafasi zao na kuwa sehemu ya baadhi ya migogoro inayoendelea Kiteto.
Aliyasema hayo mjini Kibaya akizungumza na wazee maarufu wa jamii ya wafugaji na wakulima, ili kujua kiini cha mauaji yaliyotokea Matui ambapo watu watano waliuawa kwa kukatwa mapanga.
Mbwilo alisema wapo baadhi ya viongozi kuanzia ngazi ya Kata,Vijiji na Mitaa wamebeba uongozi bila kujua dhamana zao.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI