Na Beatrice Lyimo, Maelezo.
TAKRIBANI
watu 40,000 nchini wakiwemo wanawake na wanaume wanapata ugonjwa wa
saratani kila mwaka, ambapo asilimia 12 kati yao wana saratani ya matiti
huku wengine wakiwa na saratani ya mlango wa kizazi.
Takwimu
toka Hospitali ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha kuwa kati ya
wagonjwa hao, idadi ya wanawake wanaopata ugonjwa huo kila mwaka ni
zaidi ya 3,000 ambapo idadi hiyo ni sawa na asilimia 10 ya wanaofika kwa
ajili ya matibabu hospitalini huku wengi wao wakiwa wamechelewa.
Hivi
karibuni Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania (TBCF) ilizindua kampeni
ya uchangiaji wa fedha kupitia mitandao ya simu za mikononi ikiwa ni
jitihada mojawapo ya kusaidia mapambano dhidi ya ueneaji wa magonjwa ya
saratani ya matiti na ya mlango wa kizazi.
Katika
uzinduzi wa kampeni hiyo, Jamii imetakiwa kuiunga mkono asasi hiyo kwa
kuchangia kiasi cha shilingi 1,000 kupitia mitandao ya simu ikiwemo ya
Vodacom (M-PESA namba 110011) na Tigo (TIGO PESA 0658-955-554).
Akizungumza
na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba alisema kuwa
takwimu za kuenea kwa magonjwa hayo nchini ni za kutisha hatua
inayotokana na uelewa mdogo wa jamii pamoja na ufinyu wa hospitali za
kutosha za kutibu magonjwa hayo.
Mhe.
Simba alisema kwamba, kiasi cha fedha zitazokusanywa kutoka kwa wananchi
zitatumika katika kutekeleza mipango mbalimbali ikiwemo ya kusomesha
wasichana wapatao 12 katika fani ya Onkolojia yenye lengo la kuendesha
programu ya upimaji na utoaji wa huduma nchini.
“Tunaomba
utoe elfu moja kwa ajili yako wewe mwenyewe, mtolee mwanao, mama yako,
dada yako, baba yako, mke wako na jirani, sote tuunganishe nguvu zetu
ili kupunguza ukubwa wa mateso wanayoyapata wale wote waliogundulika na
matatizo haya.
Asasi hii
ilianzishwa na inaendeshwa na wahanga wa saratani, na pia imekuwa
inasaidia watu wanaoishi na kutaabika na saratani kwa kuwapatia huduma
ya ushauri nasaha, kugharamia matibabu ya upasuaji na madawa ya homoni,
kuwapatia matiti bandia na sidiria maalumu baada ya kufanyiwa upasuaji
au kuondolewa matiti”, alisisitiza Mhe. Simba.
Mhe.
Simba aliongeza kuwa mkakati mwingine wa taasisi hiyo ni wa ujenzi wa
majengo maalum ya wagonjwa wa saratani pamoja na ununuzi wa magari yenye
vipimo vya digitali vya kupima saratani ya matiti.
Aidha
katika kukabiliana na magonjwa hayo aliiasa jamii kuchangia zaidi ya
kiwango kilichotajwa kwa kuwa taasisi hiyo ina mipango na mikakati
inayopimika na kutimizika, ambapo Serikali kwa upande wake imeweka
mazingira mazuri ya uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa hao wa saratani
nchini.
“Hawa ni
wanawake jasiri waliokuwa wahanga wa saratani ya matiti hivyo ni
Majemedari katika kupigana vita kwa niaba ya wenzao, kuonyesha njia ya
wapi tuelekeze nguvu zetu dhidi ya saratani na mbinu zipi zitumike
katika kuwasaidia wahanga, familia zao na jamii kwa ujumla” alisisitiza
Mhe. Simba.
Naye Mkuu
wa Kitengo cha Tiba toka Hospitali ya Saratani ya Ocean Road ambaye pia
ni Mshauri wa Asasi ya Saratani ya Matiti Tanzania (TBCF) Dkt. Deonista
Kombe alisema kuwa Saratani ni chembechembe ambazo si za kawaida kwani
zinazozaliana mwilini kwa haraka bila mpangilio maalum.
Dkt.
Kombe alibainisha kuwa saratani ya titi ni mabadiliko ya chembechembe
ambazo zinaathiri titi na matezi yaliyo karibu na titi, wakati saratani
ya mlango wa kizazi ni ukuaji wa chembe hai usio na mpangilio kwenye
ngozi laini inayozunguka mlango wa kizazi.
Aidha
aliongeza kuwa asilimia 40 ya aina zote za saratani zinatokana na
saratani ya shingo ya kizazi huku akifafanua kuwa taasisi hiyo imepanga
kufanya matembezi ya hisani .
Akitaja
baadhi ya vichocheo vinavyoweza kusababisha magonjwa hayo ya saratani,
alisema kwamba unene uliokithiri, matumizi ya kemikali, uvutaji wa
sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, utumiaji wa vyakula vya mafuta
kutopata mtoto ndivyo vinapelekea mtu kupata magonjwa hayo.
Asasi
hiyo imepanga kufanya matembezi ya hisani tarehe 26 Oktoba mwaka huu
ambayo yanatarajiwa kuanzia katika hospitali ya Ocean Road kwa lengo la
kuchangisha fedha kwa ajili ya kuendelea kutoa msaada zaidi kwa jamii.
0 comments:
Post a Comment