Friday, October 17, 2014

MENGI MAPYA YAIBUKA KATIKA SAKATA LA MWANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI ALIYEOLEWA *PICHA*

ILIKUWA Oktoba 7 mwaka huu, saa 1.00 asubuhi katika eneo la Mbondole, Kata ya Msongola, Wilaya la Ilala mkoani Dar es Salaam kulipozuka tafrani baada ya mwanamume mmoja kukamatwa akituhumiwa kumweka kinyumba binti mwenye umri wa miaka 15.
Mama wa binti aliyewekwa kinyumba, Amina Juma anasema mshtuko alioupata baada ya kumwona binti yake akichomoza katika chumba cha mwanamume huyo, ulisababisha tumbo lake kumkata kwa uchungu.
“Sikuamini macho yangu kumuona mwanangu akitolewa katika chumba hicho, nilitamani iwe ndoto... lakini ilikuwa kweli na tukio hilo liliniumiza sana,” anasema mwanamke huyo.
Akisimulia huku machozi yakimtoka, anasema siku hiyo alipata taarifa kutoka kwa mdogo wake kuwa mwanaye anaishi na mwanamume huyo huku akifungiwa na kufuli ndani kwa kuhofia isijulikane.
Baada ya kupata taarifa hizo, walishirikiana na mdogo wake kwenda kutoa taarifa katika ofisi ya Serikali za Mtaa huo, ili waweze kumdhibiti mtuhumiwa na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria. Katika ofisi hiyo, walisaidiwa na wajumbe wa kamati ya ulinzi ya mtaa huo, ambao walikaa kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 8:30 mchana ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo anakamatwa.
Mkasa ulivyoanza
Ilikuwa Agosti mwaka huu mama huyo akiwa nyumbani kwake alifika kijana mmoja ambaye alijitambulisha kuwa ni mshenga anayetaka kutoa posa kwa mwanaye. Hata hivyo, alimkatalia na kumweleza kuwa mtoto wake bado anasoma.
“Baada ya kumkatalia mshenga huyo akaanza kutumia mwanya wa kuja gengeni kwangu, ili amrubuni akubali kuolewa na huyo mwanamume lakini alikuwa anakataa,”anaelezea mama wa mtoto huyo.
Anasema siku moja mtuhumiwa alifika nyumbani kwake na kumweleza kuwa atahakikisha mwanafunzi huyo anafutwa shule, kwa kuwa amekwamisha mpango wake.
“Siku hiyo mtuhumiwa aliniongelea maneno ya ovyo, nilikasirika na kuamua kuingia ndani kulala... nilipoamka sikumkuta binti yangu.
“Nilijaribu kuwauliza majirani kama wamemwona, lakini sikupata jibu hivyo nililazimika kwenda kwa mtuhumiwa ili kumwangalia,” anasema.
Alipofika eneo hilo alimkuta kijana mmoja na kumuuliza kama mwanaye ameonekana lakini alimjibu hakumwona, wakati huo aliiona baiskeli ya mtuhumiwa huyo akiwa nje ikiashiria kuwa alikuwa ndani.
Anasema wakati alipokuwa anamwuliza kijana huyo, mara mtuhumiwa alitoka nje na baadaye alifuatia mwanaye.
Anasema kitendo hicho kilimuudhi na alimua kumwadhibu kwa kumchapa fimbo ndipo mtoto huyo alipotoroka na kwenda kwa baba yake mzazi ambaye anaishi Kivule, Wilaya ya Ilala.
Anasema siku ya pili alilazimika kwenda kumfuata ili wafanye kikao cha ndugu kuhusiana na suala hilo.
Baada ya kikao mtoto huyo alipoulizwa, alidai kuwa hataki tena shule.. “hivyo nilimchukua na kwenda naye nyumbani, lakini mume wangu wa sasa (baba mlezi wa binti huyo) alimkataa kutokana na tabia zake.”
Siku iliyofuata alilazimika kumrudisha kwa baba yake mzazi na kuwa tangu hapo hakujua tena taarifa zake mpaka lilipotokea hili.
“Mimi naona huu ulikuwa ni mchezo uliopangwa na mtuhumiwa na baba mzazi wa mtoto huyu, inaonekana alikuwa anajua mchezo mzima. Kama mwanaye hakuwapo nyumbani kwa nini hakutoa taarifa polisi? Au kwa ndugu?” anahoji.
Sakata latinga polisi
“Oktoba 10 mwaka huu nikiwa nyumbani kwangu, walikuja askari kutoka Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga walichukua maelezo yangu na ya mtoto na baada ya hapo waliniambia niende polisi baada ya siku tatu,” anasema.
Baada ya kutoa maelezo polisi ilifunguliwa jalada la kesi ya ubakaji lenye namba STK/RB/13749/14 na wakati huo nilipewa fomu ya polisi kwa ajili ya kwenda Hospitali ya Amana ili vichukuliwe vipimo vyote.
“Hivi unavyoniona nampeleka mwanangu katika Hospitali ya Amana ili akapime vipimo vyote ambavyo vinahitajika,” anaeleza.
Alivyomlea mwanaye
Mama huyo anasema aliachana na mumewe wa kwanza wakati binti huyo akiwa na umri wa miaka miwili na kwamba tangu wakati huo, alimlea peke yake kwa hali na mali.
Anasema alipofikisha umri wa miaka saba, alianza darasa la kwanza na hapo akaanza kumtembelea baba yake na hata kulala lakini hakuwahi kupewa fedha kwa ajili ya shule.
Binti anena
Binti huyo anasema alikutana na mwanamume huyo alipokuwa anakwenda kununua mkaa katika banda lake lililopo katika eneo hilo la Kigezi.
Anasema mwanamume huyo alikuwa akimlaghai kwa kumwambia kuwa ameshakuwa mtu mzima hivyo aache shule aolewe.
Akiwa kwa baba yake mzazi, binti huyo anasema mwanamume huyo alikuwa akivizia baba huyo anapoondoka naye anamfuata na kumweleza kuwa anataka kumpeleka mshenga, lakini baadaye alimtorosha.
“Nilianza kuishi naye mwezi uliopita, alinitorosha kutoka Kivule kwa baba yangu mzazi na kunipeleka nyumbani kwake Mbondole,” anasimulia.
Anasema wakati huo alimweleza kuwa ana watoto watatu wanaotakiwa kulelewa kwa kuwa aliachana na mama yao.
Mwanamume aliyekuwa anaishi naye alikuwa anafanya biashara ya kuuza mkaa eneo la Kigezi na kila siku alikuwa akimwachia Sh5,000 kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Viongozi wa Serikali wafunguka
Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi wa Mtaa huo, Julius Meng’anya anasema baada ya kupewa taarifa hizo walikwenda hadi kwenye nyumba hiyo ili kumkamata mtuhumiwa. Walifika asubuhi eneo kwa ajili ya kulinda na kuhakikisha mtuhumiwa huyo wanamdhibiti na ilipofika saa 8.30 mchana aliporudi nyumbani kwake walimkamata pamoja na mwanafunzi huyo.
Baada ya kumkamata walimtaarifu mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo ambaye alifika kwenye eneo hilo lakini cha kushangaza alimwachia huru mtuhumiwa huyo.
“Kwa kweli kitendo cha mwenyekiti kumwachia mtuhumiwa huyo kilituudhi sana tulitegemea mtuhumiwa angechukuliwa hatua za kisheria,” anasema Meng’anya.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo, Salum Matangula alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema mtuhumiwa alikiri mbele ya kikao kuwa alipewa ruhusa na mama mzazi wa mtoto huyo ili aishi naye.
Anasema kutokana na maelezo ya pande zote, walibaini kuwa wote wana makosa ndipo walipomtaka mama huyo aende kwenye duka la dawa ili achukuliwe kipimo cha mimba na baada ya hapo ampeleke mwanafunzi huyo shuleni.
“Niliwaeleza kuwa wote wana makosa, mama alikuwa anadai mwanaye akapime kwanza, nikamruhusu, lakini sijapata majibu hadi leo,” anasema Matangula.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kigezi anayosoma mtoto huyo, Joseph Kalungutu anasema mwanafunzi huyo ni mtoro na kipindi cha nyuma alikuwa akihudhuria darasani mara moja moja na lakini kuanzia Septemba, mwaka huu, hakuonekana kabisa shuleni.
“Mahudhurio yake ni mabaya, baada ya kuona maudhurio yake siyo mazuri nilimwita mama yake ambaye alidai kuwa hayupo anaishi kwa baba yake mzazi,” anasema Kalungutu.
Anasema Septemba mwaka huu akiwa shuleni hapo alikwenda mwanamume aliyejitambulisha kuwa mzazi wa binti huyo akidai kuwa amekwenda hapo kwa ajili ya kumfuta shule mwanaye kwa kuwa anaonekana mkubwa.
“Nilimkatalia na kumweleza kuwa sheria hairuhusu mwanafunzi yeyote aliyeandikishwa kufutwa shule hadi hapo atakapomaliza. Nilimweleza kuwa yeyote anayejaribu kufanya hivyo lazima afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Mwanamume anayedaiwa kumtorosha binti huyo, Halifa Ally anakiri kuwa aliishi naye... “Sina cha kukueleza zaidi ya hayo ninachofahamu huyo binti nilikuwa naishi naye,” anasema Ally.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki anasema Ally anayetuhumiwa kuishi na binti huyo ametoroka... “lakini polisi inawahoji mama wa mtoto huyo pamoja na mwanaye katika Kituo cha Polisi cha Stakishari huku tukiendelea kumtafuta mtuhumiwa ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria,” anasema Nzuki. Chanzo: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI