Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akizungumza kwenye mkutano na
waandishi Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema,
Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohamed.
Picha na
Venance Nestory.
KAMATI KUU ya Chadema
imeazimia kuendesha kampeni ya kupinga Katiba Inayopendekezwa kwa
viongozi wake wakuu pamoja na wale wa mabaraza yake kufanya ziara katika
mikoa mbalimbali nchini.
Hatua
hiyo imekuja siku tatu, tangu Rais Kikwete autangazie umma wa Watanzania
alipokuwa akihutubia kilele cha Mbio za Mwenge mkoani Tabora kwamba
Katiba Inayopendekezwa inafaa hivyo kuwataka Watanzania waipigie kura
wakati wa mchakato wa kura ya maoni.
Ziara ya
Chadema itaanzia katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako itachukua siku 20
ikiongozwa na Baraza la Wanawake (Bawacha), linaloongozwa na Mbunge wa
Kawe, Halima Mdee na baada ya kumaliza, itaanza ziara nyingine ya siku
20 itakayofanywa na Baraza la Vijana (Bavicha).
Dk Slaa
alisema CCM wameanza kazi ya kuwataka wananchi kupiga kura ya ‘ndiyo’ na
Chadema wanaanza mikutano ya kuwashawishi wananchi kuikataa kwa
kuipigia kura ya ‘hapana’.
Alisema kuanzia Novemba 5 mwaka huu, viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho nao wataanza ziara katika mikoa mbalimbali nchini.
“Bawacha
ndiyo itakuwa timu ya kwanza. Itakwenda Mwanza mjini, Ukerewe, Magu,
Sengerema, Geita, Busanda, Bukombe, Biharamulo, Muleba, Karagwe, Bukoba
Mjini, Chato, Shinyanga Mjini na Maswa Mashariki,” alisema Dk Slaa.
Alisema
uchakachuaji uliofanyika katika Bunge la Katiba umezaa Katiba
isiyotokana na maoni ya wananchi, kwamba kazi iliyopo sasa ni kuipigia
kura ya ‘hapana’ kwa sababu inabeba kundi fulani la watu wachache.
“Itakayopatikana
si Katiba ya Tanzania ni Katiba ya CCM. Chama hiki kiliandaa rasimu
yake na kuhakikisha kuwa inaingizwa katika Katiba Inayopendekezwa. Mwaka
2011 Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) iliagiza viongozi wa CCM kuhakikisha
kuwa mambo yote yanayopigiwa debe na chama hicho yaingizwe katika Katiba
na hilo limefanikiwa,” alisema na kuongeza:
“Tunapenda
kuwaeleza Watanzania, asasi mbalimbali na taasisi za dini kuwa wakati
umefika. Sasa tuache kulialia, kulalamika na kunung’unika.”
Tafsiri ya Katiba
Mwanasheria
Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alieleza hatua mbalimbali zinazotoa
tafsiri ya wazi jinsi Katiba Inayopendekezwa inavyokosa uhalali wa
kupigiwa kura ya ‘ndiyo’ katika kura ya maoni.
“Kwanza
Bunge Maalumu la Katiba lilijigeuza Tume ya Katiba na kuanza kukusanya
upya maoni ya makundi mbalimbali. Wajumbe waliokuwa nje ya Bunge hilo
kuruhusiwa kupiga kura na wale waliopiga baadhi ya Ibara kuhesabiwa kuwa
wamepiga kura ya ‘ndiyo’,” alisema Lissu.
Alisema
hata baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walioelezwa kuwa wangepiga kura
katika balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali, haijaelezwa walipigia
kura hizo wapi.
“Wajumbe
wa Bunge la Katiba, Mohamed Raza na Salim Turky wote kutoka Zanzibar
waliharibu kura zao, lakini zilizoharibika zilihesabiwa kura halali.
Hata hivyo Raza na Turky walipotafutwa jana kupitia simu zao za mkononi kuzungumzia suala hilo hawakupatikana.
Alisema
hata wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka Zanzibar na
wengine waliosusia vikao vya Bunge hilo na ambao hawajulikani majina yao
hadi sasa, zilihesabiwa kura halali za ‘ndiyo’.
“Maulida
Komu alikuwa Ukawa, katika Gazeti la Serikali alitangazwa anatokea
Zanzibar, aligeuzwa na kuonekana kuwa anatokea Tanzania Bara. Mjumbe
mwingine, Zakhia Meghji wa CCM anatokea Tanzania Bara lakini tumeelezwa
kuwa anatokea Zanzibar,” alisema.
Katika
hatua nyingine, wakati Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akidai
kuwapo kwa mpango wa ununuzi wa helikopta tatu za Serikali kwa malengo
ya kuzitumia kuisaidia CCM kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, Katibu Mkuu
Kiongozi, Ombeni Sefue amesema madai hayo siyo ya kweli.
Jana,
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha Kamati
Kuu ya Chadema, Dk Slaa alidai kwamba kuna mpango wa ununuzi wa
helikopta tatu za Serikali ambao unapangwa kufanywa bila kufuata
taratibu za ununuzi na kwamba Rais Jakaya Kikwete akienda ziarani China
ataiona mojawapo.
Alidai
kwamba helikopta hizo zitakazonunuliwa kwa mkopo kutoka Serikali ya
Ujerumani, zitanunuliwa Ufaransa lakini wakala anayetumika kuzinunua
anatuhumiwa nchini kwa ufisadi, alisema wakati ukifika atataja jina la
wakala huyo.
Mbali na
helikopta hizo, Dk Slaa pia alidai kuwapo kwa mpango wa kununua mitambo
maalumu ya kunasia sauti za viongozi wa Chadema.
Hata
hivyo, Balozi Sefue katika maelezo yake alisema: “Ni kweli kwamba Rais
atakwenda China kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, lakini haendi
kuangalia chopa”.
Katibu
Mkuu Kiongozi aliweka wazi kuwa yapo mawazo ya kununua helikopta hizo
kwa ajili ya matumizi ya jeshi lakini uamuzi bado haujafanyika.
“Hata
kama uamuzi utafanyika kwamba zinunuliwe kwa ajili ya kuliwezesha jeshi
letu (nasisitiza, bado uamuzi haujafanyika sasa) haiwezekani kusafirisha
helikopta kwenda China kwa sababu ziara ya Rais haihusiani kabisa na
suala hilo,” alisema.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema kauli ya Dk Slaa ni
uzushi na uongo na kwamba ajifunze kusema kweli... “Ni kiongozi na
tunamheshimu kwa hiyo lazima ajifunze kusema kweli. Haiingii akilini
kusema kwamba helikopta inaweza kusafiri kilometa zote hizo kwenda
kumfuata Rais China eti akaione, kwani Rais ni injinia au ni nani?
Halafu technically (kiufundi) ni jambo lisilowezekana”. Umbali kutoka Paris Ufaransa hadi Beijing, China ni kilometa 8,022.
Uchaguzi Mkuu
Akigusia
ununuzi wa mitambo ya usalama itakayotumiwa na Jeshi la Polisi, huku
akionyesha nyaraka ya serikali yenye maelezo ya ununuzi huo iliyoandikwa
na Ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (jina
limehifadhiwa) alisema:
“Rais
ameomba kwenda Beijing kwa ajili ya kuona mitambo ya kiusalama ya
polisi. Cha kushtusha zaidi katika nyaraka hii inaeleza mitambo hiyo
lazima iwe imefika haraka iwezekanavyo kabla ya Uchaguzi Mkuu kwa sababu
tunaogopa kuna vurugu zitatokea. Hayo yamesemwa kwenye maandishi wa
Serikali,” alisema.
Alisema
aliyeandikiwa nyaraka hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na kufafanua kuwa
nyaraka hiyo iliandikwa Oktoba7, 2014 na mawasiliano kati ofisa huyo na
Waziri yalifanyika saa 11 jioni.
Katika
mkutano wake Dk Slaa pia alisema: “Rais anaambiwa kwamba ndege ya Jeshi
anayotaka kununua ipo kwenye mji mwingine, mji huo haupo katika eneo la
ziara yake, lakini wanawaambia wahusika kule China, ndege irushwe na
iletwe mpaka Rais atakapokuwa ili aione mwenyewe. Hivi Rais ni ofisa
mnunuzi au!” alihoji.
Akizungumzia
hilo safari hiyo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Mkumbwa Ally
alisema: “Hatuna taarifa kama Rais anakwenda Beijing.”
Kuhusu
madai ya Rais kukagua vifaa vya kiusalama vya polisi na helikopta
zinazodaiwa kuwa zitanunuliwa Mkumbwa alisema: “Hayo ni madai ya
kufikirika kwa kuwa Rais siyo ofisa ununuzi.”
Chanzo: Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment