Thursday, August 14, 2014

WAUGUZI WATUMIA TOCHI KUZALISHIA WAJAWAZITO ULANGA MKOANI MOROGORO

WAUGUZI wa Zahanati ya Kivukoni, Kata ya Minepa, Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro, wanalazimika kutumia tochi kushona majeraha na kuzalisha wajawazito wanaofika kupata huduma usiku.

Afisa afya zahanati hiyo, Costansia Mpangile aliwaeleza waandishi wa habari kituoni hapo kuwa hali hiyo inatokana na kukosekana kwa umeme.

Mpangile alisema wanalazimika kutumia tochi wanazotoka zao binafsi kwa ajili ya kupata mwanga wakati wa kuwahudumia wajawazito wanaohitaji kujifungua kwa dharura usiku na wagonjwa wanaohitaji kushonwa majeraha.

Alisema kuwa hali hiyo inatishia usalama wa utoaji wa huduma na hasa ikizingatiwa kuwa zahanati hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka vijiji mbalimbali vya ndani na nje ya kata hiyo.

“Kama umeme ungekuwepo ungesaidia tuwe na majokofu ya kuhifadhi chanjo na kuondoa mzigo kwa wananchi kufuata huduma hizo makao makuu ya tarafa kwenye kituo cha afya ambacho kiko mbali.

“Kwa siku tunapokea wagonjwa 30 hadi 40, wakati wa usiku ndio inakuwa ngumu kutoa huduma kwani umeme hakuna na hivyo hatari sana kwa wagonjwa wetu,”alisema.

Alisema iwapo serikali itatilia mkazo changamoto hiyo kwa haraka, kuna uwezekano mkubwa wa kusaidia kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto, sambamba na kuboresha zaidi utoaji wa huduma.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara, baadhi ya wananchi wa Kivukoni, Sofia Msalata na Salum Mnyambule walisema pamoja na kujisajili kwenye mifuko ya afya ya jamii, bado huduma zinazotolewa katika zahanati hiyo haitoshelezi.


Naye  mbunge wa Ulanga Magharibi, Dk. Haji Mponda, alisema tayari waliisukuma Serikali kuona changamoto hiyo na ilitenga sh. milioni saba kwaajili ya kufikisha umeme katika zahanati hiyo lakini kinachokwamisha hivi sasa ni utaratibu wa mfumo wa malipo ya serikali.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI