Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
AKIZUNGUMZIA kauli hiyo na kituo cha Radio One jana asubuhi, Mbowe alisema: “Nashindwa kujua Waziri Mkuu akizungumzia Ukawa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa alikuwa akizungumzia kwa namna ipi, nashindwa kumwelewa.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameelezea kushangazwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwamba kitendo cha Ukawa kususia Bunge la Katiba kinauweka njia panda uchaguzi wa serikali za mitaa.
Kauli ya Mbowe inatokana na
Pinda kusema juzi kuwa hatma ya uchaguzi huo itategemea uamuzi wa wajumbe wa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) kurejea katika Bunge Maalum kuipitisha Katiba Mpya kwa wakati.
Waziri Pinda alisema hayo wakati akizungumza na mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya na miji nchini uliofanyika jijini Tanga, ikiwa ni sehemu yamaadhimisho ya Wiki ya Serikali za Mitaa yaliyofanyika kitaifa mjini Tanga.
Akizungumzia kauli hiyo na kituo cha Radio One jana asubuhi, Mbowe alisema: “Nashindwa kujua Waziri Mkuu akizungumzia Ukawa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa alikuwa akizungumzia kwa namna ipi, nashindwa kumwelewa.
“Mabadiliko ya sheria ambayo ni muhimu kufanyia marekebisho kabla ya uchaguzi, hayafanywi na Bunge la Katiba, yanafanywa na Bunge la kawaida, kwa sasa hakuna Bunge na Bunge la kawaida linatarajia kukaa Novemba 4 mwaka huu, kipindi ambacho uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakuwa umeshapita.
“Kwa maana hiyo, kuanzia sasa hadi Novemba, Bunge halitakutana kama bunge la kawaida, kwa hiyo hakuna fursa ya mabadiliko ya sheria yoyote ile hadi Novemba, labda kuwe na Bunge la dharura, sasa Waziri Mkuu anaposema kutorejea kwa wajumbe wa Ukawa katika Bunge la Katiba kutakwamisha uchaguzi, si kweli.
“Serikali yenyewe imechelewa kuleta muswada wa marekebisho ya sheria. Imechelewa kurekebisha kanuni na sasa inataka kuleta kisingizio cha nini kinachelewesha na kuwa wajumbe wa Ukawa ndiyo wanachelewesha. Lakini hivi (uchaguzi na Ukawa) ni vitu viwili tofauti,” alisema.
Kurejea bungeni
Akizungumzia mustakabali wa Ukawa kwenye Bunge la Katiba baada ya kuwepo wito wa watu mbalimbali, wakiwamo za viongozi wa dini, Mbowe alisema kuwa watu wanatafsiri vibaya kuwa wajumbe wa umoja huo wanagoma kurejea kwenye Bunge la Katiba, kinachotakiwa ni kuangalia sababu gani zinawafanya kushikilia msimamo huo.
Alifafanua kuwa wakati wanagomea Bunge la Katiba walikuwa na sababu za msingi na bado zipo, hazijatatuliwa wala hazijafanyiwa kazi. Kwa maana hiyo, kwa kuwa hazijafanyiwa kazi na hazijatatuliwa, wataendelea kubaki nje ya Bunge.
Hata hivyo, Mbowe alisema kuwa msimamo wao kugomea Bunge la Katiba siyo wa kudumu kwani unasababishwa na mazingira.
“Watu wakae chini, watathmini, waangalie matatizo yako wapi na tutatue matatizo mapema na yakikamilika, watu watarejea bungeni. Lakini hatuwezi kurudi pale kwenda kutukanana, kunyanyasana na kuvunjiana heshima. Haileti maana kabisa, kitu ambacho si malengo ya Bunge la Katiba.
“Msimamo wetu (wa kususia Bunge la Katiba) si wa kudumu, unasababishwa na mazingira. Watu wakae chini, watatue matatizo na yakimalizika watu watarejea bungeni...lakini kama hatukutatua, itakuwa ni kama watoto wadogo wasiofanya tathmini wala kujua athari ya kitu,” alisema.
Kauli za msajili
Kuhusu nafasi zao kwenye vyama kuwa hawana sifa na wanabanwa na katiba kama ilivyosema ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Mbowe aliponda kauli ya hiyo akisema kuwa anaweza kuzungumza chochote na kwa kuwa msajili si mahakama, anaweza kutoa tafsiri yake kwa mtazamo wake, lakini uhalisia utaonekana katika vyombo husika.
Akizungumzia kuhusu ukomo wa uongozi na madai kwamba walibadilisha kinyemela kipengele hicho katika Katiba, Mbowe alisema si wakati muafaka kujiingiza kwenye malumbano yasiyo na maana.
wa juu pekee kama ilivyoelezwa.
“Hili nalitazama katika sehemu mbili: Kwanza; kama ukomo ni kwa viongozi wote wa nchi nzima katika nafasi mbalimbali, mikoa hadi kata, na wapo viongozi wametumikia chama kwa zaidi ya miaka 10 hadi 15 na sheria zinatungwa si kwa ajili ya mwenyekiti na katibu wake.
“Pili; uamuzi wa ukomo na nani aongoze taasisi kwa muda gani wanaamua wanataasisi kupitia vikao na kama inasemwa mkutano mkuu uliridhia vinginevyo, sijui msajili alikuwa na maana gani. Lakini si wakati mwafaka kujiingiza katika malumbano yasiyokuwa na maana,” alisema Mbowe.
Kuhusu malalamiko kwa viongozi kutotimiza majukumu ya chama, alisema viongozi wanaolalamika kutotekelezwa mambo mbalimbali ni wasaliti kwa kuwa mambo ya chama yanazungumzwa ndani ya vikao halali.
“Kwa sasa ni wakati wa kwenda kwenye uchaguzi na mahasimu wanafanya mbinu mbalimbali kukidhoofisha chama na ninataka kusema kuwa chama kiko imara na hao wanaotaka kuleta chokochoko za kitoto na mambo ya kijinga, hawatakuwa na nafasi,” alisema Mbowe.
“Tumetoka hatua moja kwenda nyingine. Kwa muda mrefu, tumekiimarisha chama kwa gharama kubwa na tutakilinda chama kwa gharama zote. Chama hiki kinaheshimu katiba, kinapigania haki na ustawi wa Tanzania.
“Hatutatetereka kwa watu wachache wanaotumika kwa mbinu mbalimbali eti kukipaka matope chama ili chama kiingie kwenye uchaguzi tukiwa tumejeruhiwa. Hatutaogopa kikundi chochote kinachoandaliwa kimkakati kuichafua Chadema na tutapambana nacho.”
MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment