Novemba 9, 2012
UCHAGUZI TAREFA, TAFCA SASA DESEMBA 22
Uchaguzi
wa viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) na
Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) sasa utafanyika
Desemba 22 mwaka huu.
Kwa
mujibu wa ratiba za uchaguzi za vyama hivyo, Kamati zao za uchaguzi
zitatangaza kuanza mchakato wa uchaguzi Novemba 10 mwaka huu wakati fomu
kwa wanaotaka kugombea uongozi zitaanza kutolewa Novemba 12 mwaka huu.
Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Novemba 16 mwaka huu.
Kamati
ya Uchaguzi ya Shirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa
mwongozo huo kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA baada ya kuomba hivyo
kutokana na wagombea sita tu kujitokeza kuomba nafasi tatu za uongozi
katika mchakato wa awali.
Kwa
waombaji ambao awali walichukua na kulipia ada ya fomu za kugombea
uongozi TAFCA na TAREFA, hawatatakiwa kulipia tena ada kwa nafasi zile
zile walizoomba, isipokuwa watatakiwa kujaza fomu upya.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA FA MWANZA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) uliochaguliwa katika
uchaguzi uliofanyika Novemba 8 mwaka huu.
Ushindi
waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa MZFA walivyo na imani kubwa kwao katika
kusimamia mchezo huo katika Mkoa wa Mwanza.
TFF
inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati za Utendaji ya MZFA
iliyochaguliwa chini ya uenyekiti wa Patrick Songora aliyechaguliwa kwa
kipindi cha pili mfululizo.
Uongozi
huo mpya wa MZFA una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha
unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya chama
chao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
Pia
tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na Kamati ya Uchaguzi ya
TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi
waliochaguliwa kuongoza MZFA ni Patrick Songora (Mwenyekiti), Nassoro
Mabrouk (Katibu) na Richard Kadutu (Mwakilishi wa Klabu TFF).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 comments:
Post a Comment