Picha zote na Habari na Francis Gwodin Mzee wa matukio
KUFUATIA kuvamiwa kwa makanisa matatu mkoani Iringa na kujeruhiwa kwa paroko wa parokia ya Ismani mkoani Iringa, Rais Dkt. Jakaya Kikwete amemfariji paroko Angelo Burgeo (60) na msaidizi wake Herman Myalla (36) waliojeruhiwa na majambazi huku akiziomba taasisi za dini kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuimarisha ulinzi katika maeneo yao kama njia ya kukomesha matukio ya ujambazi yanayofanyika katika maeneo ya taasisi za dini.
Rais Dkt. Kikwete ametoa wito huo kupitia waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera), William Lukuvi ambaye ni mbunge wa jimbo la Isimani mkoani Iringa ambako paroko huyo na mwenzake walivamiwa, ametoa wito huo leo katika hospitali ya mkoa wa Iringa alipokuwa akiwasilisha salamu za Rais Jakaya Kikwete na kutoa pole kwa Paroko Angelo Burgeo (60) na msaidizi wake Herman Myalla (36) wa Kanisa Katoliki Parokia ya Isimani, wilayani Iringa.
Novemba 15, mwaka huu mapadri hao ambao wamelazwa katika hospitali ya mkoa wa Iringa wakiendelea na matibabu, walivamia na kushambuliwa kwa silaha za moto, mapanga na nondo na majambazi.
Watu watano wanaoshikiliwa na polisi wakihusishwa na uhalifu huo katika tukio hilo ambalo mapadri hao mbali na kujeruhiwa vibaya waliibiwa zaidi ya sh Milioni 3.8.
Akiwasilisha salamu za Rais, Lukuvi alisema ametumwa kutoa pole kwa wahanga hao, waumini na viongozi wa dhehebu hilo la dini kwa ujumla wake.
“Tupo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu ambacho majambazi wamekuwa wakiwavamia viongozi wa dhehebu hili la dini wakiamini mmehifadhi fedha na mali nyingine nyingi ndani ya parokia zenu,” alisema.
Alisema tukio la mapadri hao kuvamiwa na kujeruhiwa mkoani Iringa limekuja miezi michache baada ya matukio kama hayo kutokea katika parokia za Migori na Pawaga mkoani Iringa.
“Serikali imefanya kazi ya kutoa mafunzo kwa mgambo wengi karibu katika kila kijiji, ni wajibu wa taasisi hizi za dini kuwatumia hao au vinginevyo ikubali kushirikiana na jeshi la Polisi kutoa mafunzo kwa walinzi wao,” alisema.
Akipokea salamu hizo, Padro Burgeo alisema majambazi hao walifanikiwa kuingia ndani ya parokia yake baada ya kutumia lango la nyuma na kufanikiwa kuwapiga chenga walinzi wao.
Alisema katika tukio hilo ilikuwa afe lakini Mungu amesaidia kuyanusuru maisha yake baada ya kufikishwa mikononi mwa madaktari.
Kaimu wa Mganga Mkuu wa Mkoa Dk Faustine Gwanchele amesema baada ya kumfanyia upasuaji na kutoa risasi tatu kwa Padri Burgeo hali yake inaendelea vizuri pamoja na kusumbuliwa na ugonjwa wa kisukari.
0 comments:
Post a Comment