Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo.
*******
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam.
HALMASHAURI
ya Geita itaanza kupata wastani wa Dola za Marekani milioni 1.8 kwa
mwaka kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) baada ya kusainiwa rasmi
kwa marekebisho ya mkataba baina ya kampuni hiyo na Serikali.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kabla
ya kutiliana saini marekebisho ya mkataba huo ambao uliosainiwa awali
mwaka 1999. Awali, Halmashauri hiyo ilikuwa ikipata ushuru wa huduma
wa Dola za Marekani 200,000 kila mwaka badala ya kulipwa asilimia 0.3
ya mapato ghafi ya kila mwaka kama sheria ya fedha ya serikali za
mitaa ya mwaka 1982 inavyotaka.
Kwa
kuzingatia kiwango cha mapato ghafi ya mgodi wa Geita kwa mwaka
yanayopatikana hivi sasa, Halmashauri ya Geita itakuwa na uhakika wa
kupata kiasi kisichopungua Dola za Marekani milioni 1.8 kwa mwaka.
Kwa
mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na wamiliki wa
mgodi huo, malipo hayo yataanza kulipwa rasmi kuanzia tarehe 01 Julai,
2014.
Profesa
Muhongo alisema kuwa fedha hizi ni nyingi mno na kuwataka wananchi wa
Geita kujiandaa kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu pamoja na huduma
za jamii zitakazopelekea uchumi wake kukua kwa kasi.
Profesa
Muhongo alisisitiza kuwa ni vyema makabidhiano ya fedha hizo kwa njia
ya hundi yakafanyika kwa uwazi mbele ya wananchi ili kupunguza
malalamiko, ikiwa ni pamoja na kuongeza imani kati ya wananchi na
migodi.
Aidha,
aliwataka Viongozi wa Halmashauri hiyo, kusimamia vyema fedha hizo
kwa kuhakikisha kuwa zinachangia katika shughuli za maendeleo badala ya
kutumika katika matumizi yasiyo ya lazima na tija katika jamii, hususani
kulipana posho za vikao na safari.
“ Kwa
mazingira ya sasa, mji wa Geita hauna sababu ya kukosa maji, barabara
bora, vituo vya afya, ni imani yangu kuwa fedha hizi zitachangia kwa
kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa Geita iwapo zitasimamiwa
ipasavyo,” alisema.
Maeneo
mengine yaliyofanyiwa marekebisho kwenye mkataba wa awali
uliosainiwa mwaka 1999 ni kupandisha kiwango cha malipo ya mrabaha
kutoka asilimia tatu ya mapato baada ya kuondoa gharama za uchakataji
madini na kufikia asilimia nne ya mapato ghafi.
Eneo
jingine lililofanyiwa marekebisho ni kufuta kipengele kilichokuwa
kinatoa nyongeza ya asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao
haujarejeshwa. Kuendelea kuwepo kwa kipengele hiki kwenye mkataba,
kungeipunguzia serikali kodi ya mapato.
0 comments:
Post a Comment