Thursday, September 25, 2014

"TUMEPOTEZA MECHI YA KWANZA, HATUTAKI KUPOTEZA YA PILI" - MURAGE KABANGE

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KAGERA SUGAR imejificha jijini Dar es salaam kujiwinda na mechi ya raundi ya pili ya ligi kuu soka Tanzania bara itakayopigwa jumapili (septemba 28 mwaka huu) dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange amesema baada ya kupoteza mechi ya kwanza 1-0 dhidi ya JKT Mgambo katika uwanja CCM Mkwakwani jumamosi iliyopita, hawatakuwa tayari kuacha pointi tatu mbele ya maafande hao wa Pwani.
Mechi hiyo inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na ubora wa kikosi cha Fred Felix Minziro kilichotoka suluhu pacha ya bila kufungana na Mbeya City fc katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu jumamosi iliyopita uwanja wa CCM Sokoine, Mbeya.
JKT Ruvu ilionekana kuwa na nidhamu ya hali ya juu ya mchezo, na Minziro alisema timu yake ilicheza vizuri na sasa wanaipigia hesabu Kagera Sugar.
Lakini Kabange wa Kagera Sugar alisema: “Tumerudi na tuko hapa Dar es salaam tangu jumatatu. Vijana wanajitahidi katika mazoezi na tutahakikisha tunafanya vizuri.”
“Mechi iliyopita tulijikwaa kidogo, tulipata nafasi za kufunga pamoja na penalti, lakini hatukufanikiwa kufunga. Tunarekebisha matatizo ya kikosi chetu na tunaamini mechi ijayo dhidi ya JKT Ruvu tutafanya vizuri.”
“Mpira umebedilika duniani kote, unaweza kushinda mahali popote, tunajua ugumu wa wapinzani wetu, lakini tumejipanga. Tumepoteza mechi ya kwanza na hatutaki kupoteza mechi ya pili”.

0 comments:

Post a Comment

ZILIZOSOMWA ZAIDI