Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Kisemu Morogoro vijijini waakiimba kwaya.
Picha ya maktaba MTANDA BLOG.
*****
TANZANIA ni moja ya nchi zitakazonufaika na ushirikiano mpya wa kimasomo, uliosainiwa jijini hapa juzi kwa lengo la kuwasaidia wasichana kujikita katika nyanja za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.
Katika ushirikiano huo, miongoni mwa manufaa yake ni kutoa fursa kwa wasichana, watakaofanya vizuri kimasomo kusoma katika vyuo vya elimu ya juu nchini Marekani.
Hayo yalifahamika juzi wakati wa utiaji saini ushirikiano huo, ambako Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko hapa kwa ziara ya kikazi ikiwa pamoja na kuhudhuria vikao vya Umoja wa Mataifa, alielezea kufurahishwa kwake na mpango huo.
Rais alisema ni ukweli kwamba kuna tofauti kubwa ya uwiano wa kijinsia katika masomo ya Sayansi na Hisabati, kati ya nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea.
“Lakini tofauti ni kubwa zaidi kwa nchi zinazoendelea. Kama zilivyo katika nchini nyingi, ikiwamo Tanzania, wasichana ni wachache mno katika nyanja zilizolengwa,” alisema.
Alisema hali hiyo ni ya kihistoria na alitoa mfano kuwa Tanzania kabla ya Uhuru, wakati huo ikiitwa Tanganyika, ilikuwa na shule mbili tu kwa ajili ya kusomesha watoto wa machifu na watumishi wa serikali ya kikoloni.
Alisema kutokana na hali hiyo, nchi ilijikuta ikiwa na wahandisi watatu na madaktari wanne tu, wote wa kiume wakati nchi inapata uhuru mwaka 1961.
Hata hivyo, alisema tangu baada ya Uhuru, Serikali imefanya juhudi kubwa za kuwekeza katika elimu, ikilenga kutoa fursa za kielimu bila ya ubaguzi wa kijinsia.
“Bado tuna uhaba wa wanasayansi, wahandisi na mabingwa wa hisabati. Kwa mfano, tuna wahandisi 7,000 waliosajiliwa,” alisema.
Kutokana na tofauti hiyo, alisema Serikali imesomesha walimu wengi wa sayansi, ikiwa pamoja na kununua vifaa vya kufundishia, kutoa fursa za watoto wa kike ufadhili wa masomo ya sayansi, ufadhili kwa masomo ya udaktari, lakini pia fursa ya ajira kwa wote wanahitimu masomo yao katika maeneo hayo.
Mbali ya kuhakikisha shule za sekondari za Kata, zinaongeza udahili wa wanafunzi kutoka 524,000 mwaka 2005 hadi milioni 1.9, Serikali inahakikisha pia kila shule inakuwa na maabara.
Alisema tayari kuna mafanikio makubwa ya kuondoa pengo la wanafunzi kati ya wavulana na wasichana, licha ya kuwapo kwa changamoto za ujauzito na ndoa za utotoni miongoni mwa watoto wa kike.
Awali, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC) , Dk Nkosazana Dlamini- Zuma alisema miongoni mwa mikakati ya umoja huo na Afrika ni kuondoa tofauti za kijinsia katika elimu, hasa ya sayansi na teknolojia, kama njia mojawapo ya kumsaidia mtoto wa Afrika kupiga hatua katika maendeleo.
Chanzo: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment