Waziri Mkuu Mizengo Pinda
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU

*Asihi viongozi, watumishi wa umma wasiache kumuomba Mungu
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema
anamshukuru Mungu kwa kumuwezesha kumaliza salama utumishi wake
Serikalini kwenye ngazi za juu ambao umedumu kwa takriban miaka 15.
Akizungumza na waumini wa Kanisa
Katoliki wakati wa Ibada ya Jumapili katika Parokia ya Mt. Anna iliyoko
Hananasifu, Kinondoni leo mchana (Jumapili, Oktoba 18, 2015), Waziri
Mkuu Pinda amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia
Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na miezi tisa; pia katika
ngazi ya uwaziri miaka miwili na nusu na miaka mitano akiwa Naibu
Waziri.
“Ninamshukuru Mungu kwa
kuniwezesha kumaliza uongozi wangu Serikalini. Ninamaliza uongozi wangu
kwa amani na furaha. Katika ibada hii ya shukrani nimemuomba Mungu
anisamehe kwa matamshi niliyoyatoa nikiwa kiongozi… yanaweza kuwa
yaliwaudhi watu bila mimi kujua,” alisema.
“Uwaziri Mkuu ni kazi ngumu yenye
changamoto nyingi. Nitakuwa mtu wa ajabu nisipomshukuru Mungu kwa
uongozi wake katika kipindi chote hicho tangu nikiwa Naibu Waziri hadi
kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu,” alisema.
“Wito wangu kwa Watanzania wote ni
kwamba msiache kumtaguliza Mungu maishani kwa sababu yeye ndiye mtoaji
wa yote. Wote tuendelee kumtii Mungu na viongozi wetu wa kiroho kwa
sababu wako hapa kumwakilisha yeye,” alisema.
Alisema wako baadhi ya watu ambao
wakipata madaraka wanaona kwenda kanisani ni kero au ni kupoteza muda.
“Tatizo lao ni kutojijua, hawatambui kwamba bila Mungu hizo nafasi
wasingezipata. Ninawaomba tujue kwamba kuna maisha hata nje ya utumishi
wa umma na utumishi wa kisiasa,” alisema.
Alisema katika utumishi wake wa
umma amejifunza mambo mengi lakini kikubwa alichobaini ni kujua jinsi ya
kuishi na watu. “Elimu kubwa ni kujua jinsi ya kuishi, hii ni elimu
zaidi ya kitabuni,” alisema. Alitumia fursa hiyo kumshukru mke wake,
Mama Tunu Pinda kwa kuwa nguzo ya familia na kuwalea watoto wote
walionao wakati yeye akihangaika na masuala ya kitaifa.
Katika hatua nyingine, Abate
Thadei Mhagama kutoka Abasi ya Hanga iliyoko Songea ambaye aliongoza
ibada hiyo, aliwataka waumini wote nchini wazidishe sala kwa kufunga na
kuomba katika siku saba zilizobakia kabla ya uchaguzi mkuu kwa sababu
hali ni tete.
“Ninawaomba waumini wote tuzidishe
sala ili kwanza pawe na amani na upendo na pia Mungu atuwezeshe kupata
viongozi aliowandaa kwa maana ya Rais, Wabunge na Madiwani.”
“Sote ni mashahidi, tumeona kwenye
mikutano kila mgombea akija sote tunajaa huko… hii ni kwa sababu
hatujuia yupi ni yupi, ndiyo maana nasisistiza kuwa tumuombe Mungu
atuletee yule ambaye amemuandaa,” aliongeza.
Alisema kila mwananchi amesikia
kwamba uchaguzi ukishafanyika awe tayari kupokea matokeo. “Tumeambiwa
mara kadhaa tuwe tayari kukubali matokeo… kwa vile tunamuomba Mungu kwa
bidii, itakuwa rahisi kukubali hayo matokeo kuliko kwa wale ambao
wanaenda bila kuongozwa na Mungu,” alisema.
“Litakuwa jambo jepesi kwetu
kukubali matokeo kwani tutasema Mungu amemleta yule aliyemuandaa, yule
ambaye tumekuwa tukimuomba atuletee,” alisisitiza.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Baraza la Walei la Parokia hiyo, Bw. Arbogasti Warioba alisema kama
kanisa wao wanamshukuru Mungu kwa ulinzi aliompatia Mhe. Pinda kwa
kipindi chake chote cha Uwaziri Mkuu.
“Sote tunatambua kuwa kazi ilikuwa
ngumu, misafara ilikuwa ni mingi na wakati mwingine ya mwendo mkali
lakini Mungu alikutetea na kukulinda hadi leo uko salama. Tunakushukuru
pia kwa ushirikiano ulioendelea kutuonyesha wakati ukiwa madarakani na
tunakuombea uendelee kuwa na uchaji wa Mungu katika maisha yako ya
uraiani,” alisema Bw. Warioba.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.L. P. 3021,
11410
DAR ES SALAAM
JUMAPILI, OKTOBA 18, 2015.






0 comments:
Post a Comment