Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
*****
Na Muhibu Said, Jimmy Mfuru na Leonce Zimbandu.
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimelaani vikali kitendo cha polisi kuwapiga waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia tukio la kuhojiwa na polisi Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, Alhamisi wiki iliyopita.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, amesema kitendo hicho ni cha uvunjaji wa katiba ya nchi inayotoa uhuru wa kutafuta na kupata habari na pia ni cha uvunjaji wa haki za binadamu na kwamba, kimeonyesha jinsi jeshi hilo lisivyoheshimu haki za wananchi na lisivyofanya kazi yake kwa weledi.
Prof. Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa, CUF wanaunga mkono kauli ya Mbowe kupinga matumizi mabaya ya fedha za umma yanayofanywa na Bunge hilo wakati likijua kuwa katiba mpya haiwezi kupatikana.
Alisema Mbowe ana haki ya kueleza hilo na pia anaunga mkono hatua yake ya kutangaza kufanyika kwa maandamano, kwani alifuata taratibu zote za kisheria.
Prof. Lipumba alisema suala la maandamano ni moja ya haki zinazotolewa na sheria namba 5 ya mwaka 1992 inayoruhusu vyama vya siasa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara.
Alisema katika kutekeleza hayo, haki ya polisi ni kupewa taarifa ili watoe ulinzi na siyo kuombwa kibali cha kuruhusiwa kufanya maandamano kama Jeshi la Polisi linavyotaka.
“Jeshi la Polisi limejipa mamlaka ya kuzuia maandamano na mikutano ya vyama vya siasa. Polisi hawana mamlaka ya kuzuia. Maana polisi wanaotakiwa kulinda maandamano ni wachache kuliko wanaozuia,” alisema Prof. Lipumba.
Aliongeza: “Jeshi la Polisi limekuwa chanzo cha kuleta vurugu za kisiasa nchini.”
AONYA UCHAGUZI WA MITAA
Katika hatua nyingine, CUF kimesema kuna hatari nchi ikakumbwa na vurugu iwapo uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliotangazwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu, utafanyika, huku vyama vya siasa, hususan vya upinzani, vikiendelea kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara.
Kutokana na hali hiyo, CUF imemuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati na kutengua amri hiyo, ili kuepusha hali mbaya inayoinyemelea nchi wakati wa uchaguzi huo.
Prof. Lipumba, alisema hatua hiyo siyo tu itaweka sawa hali ya hewa, bali itamsaidia pia Rais Kikwete kumaliza vizuri kipindi chake cha miaka 10 ya uongozi wa nchi, kwa kuwa wenzake wanaomzunguka na kumshauri, wanamtakia mabaya.
“Hali inazidi kuwa mbaya katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa…tunamuomba mheshimiwa Rais aruhusu shughuli za kisiasa ili amalize vizuri kipindi chake. Wenzake hawamtakii mema,…maana kinachohitajika ni vurugu na vurumai zitokee nchini,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema amri ya kuvizuia vyama vya siasa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara katika mikoa ya Lindi na Mtwara, imevuka mipaka, kwani hivi sasa imekuwa ikitekelezwa pia na Jeshi la Polisi katika mikoa mingine nchini.
Alitoa mfano wa namna yeye (Prof. Lipumba) na baadhi ya viongozi wake katika chama walivyozuiwa kwa maandishi na jeshi hilo kufanya mikutano ya hadhara wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani na katika wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, hivi karibuni.
Hata hivyo, alisema wakati vyama vya upinzani vikizuiwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na baadhi ya vigogo serikalini wamekuwa wakiruhusiwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kwa mfano wafuasi wa CCM waliruhusiwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara mjini Dodoma na maeneo mengine katika mikoa mbalimbali nchini, kuunga mkono na kupongeza hotuba ya Rais Kikwete, aliyoitoa wakati akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba, Machi, mwaka huu.
Alisema kuna mmoja wa vigogo mwanamke serikalini amekuwa akifanya ziara zinazoshirikisha msafara wa pikipiki wilaya ya Lindi Vijijini, lakini hakuna aliyemzuia.
“Lakini leo vyama vya upinzani vinazuiwa. Hii ni kunyima haki vyama vya siasa tena katika kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema viongozi wa vyama vya siasa walipokutana na Rais Kikwete hivi karibuni, pamoja na mambo mengine, walimlalamikia kuhusu amri hiyo na kujibiwa naye (Rais Kikwete) kuwa hata yeye hajui ni nani aliyetoa amri ya kuzuia mikutano ya hadhara kufanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Hata hivyo, alisema Rais Kikwete katika kikao hicho aliagiza kufanyika tathmini ili shughuli za vyama vya siasa ziendelee katika mikoa yote nchini.
Lakini akasema pamoja na agizo hilo, hadi sasa vyama hivyo bado vinaendelea kuzuiwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara, kinyume cha haki ya kikatiba na kisheria. Alisema suala hilo liliwahi kupelekwa pia na vyama hivyo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye alizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP).
Hata hivyo, alisema IGP na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, wote kwa nyakati tofauti, nao pia walidai kuwa hawajui amri ya kuzuia mikutano ya hadhara kufanyika ilitolewa na nani katika mikoa hiyo.
Alisema wakati serikali ikiwa imekwisha kutangaza kwamba, uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, utafanyika Desemba 14, mwaka huu, hadi sasa vyama vya siasa vilikuwa bado havijapewa taarifa zozote kuhusu suala hilo.
Vilevilele, alisema vyama hivyo pia bado havijapewa kanuni zitakazotumika kwenye uchaguzi huo na wakati huo huo vyama vya siasa vinazuiwa kufanya mikutano ya hadhara.
“Sasa huu uchaguzi utafanyikaje? Hii serikali inataka kutuletea vurugu za nini?” alihoji Prof. Lipumba.
Alisema ana wasiwasi kwamba, kinachofanyika huenda ni mbinu za Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutaka ‘kuuchakachua’ uchaguzi huo ili CCM ishinde kwa kishindo, halafu aonekane kuwa ni hodari, apate kuungwa mkono na chama kimpe ridhaa na kumteua kugombea urais mwaka 2015.
NCCR-MAGEUZI YALAANI POLISI
Chama cha NCCR –Mageuzi kimelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kushambulia waandishi wa habari na kusema kuwa nguvu iliyotumiwa na serikali haiwezi kuleta utulivu bali itahatarisha usalama wa nchi.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Leticia Mosore, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Alisema haitawezekana kujenga Taifa bora linaloheshimu misingi ya utawala bora kwa kutumia nguvu na kuwanyamazisha raia kwa kutumia nguvu za Jeshi la Polisi.
Alisema kwamba serikali inapaswa kutambua na kuheshimu haki za binadamu.“NCCR-Mageuzi tunataka Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, kutoa tamko la uwajibikaji, ikiwa Rais hatamwajibisha kutokana na kukithiri vitendo vya Polisi kutumia nguvu,” alisema.
Mosore alisema kuwa tukio hilo la Septemba 18, mwaka huu siyo la kwanza nchini, na kutolewa mfano tukio la mwaka 2005 la Mwandishi Christopher Kidanka na mwenzake walipokuwa kazini kuripoti tukio la kuhamishwa kwa wakazi wa nyumba za ATCL Ukonga na walipigwa na kuharibiwa vitendea kazi vyao.
“Tukio lingine la kutisha ni lile la Daudi Mwangosi lililotokea Septemba 2, 2012 la kuuawa kwa bomu lililotupwa na askari wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa,” alisema.
Alisema vitendo kama hivyo ni ushahidi wa kukithiri kwa matumizi mabaya ya nguvu za dola dhidi ya raia na wanahabari.
CHADEMA: CHAGONJA AWAJIBISHWE
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kuwapiga waandishi wa habari wakiwa katika kutekeleza majukumu.
Aidha, wametaka Kamishana wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo, Paul Chagonja, achukiliwe hatua kwa kuwa alikuwa akishuhudia tukio hilo la waandishi kupigwa.
Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaila, alisema kitendo walichofanyiwa waandishi siyo kizuri kwa kuwa walitaka kuihabarisha jamii kuhusu kilichokuwa kinaendelea baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwenda kuhojiwa na polisi kwa sababu ya kutangaza maandamano nchi nzima kushinikiza Bunge la Katiba kusitishwa.
Katika hatua nyingine chama hicho kimesema maandamano ya nchi nzima kushinikiza Bunge hilo kusitishwa liko palepele kwa kuwa ni maazimio ya mkutano mkuu wa chama hicho na kwamba sababu za Jeshi la Polisi za kuyasitisha hazina mashiko.
Kigaila alisema maandamo hayo yatakuwa ya wiki nzima kuanzia leo hadi Jumamosi na watakutana katika ofisi za wakuu wa mikoa na wilaya.
Alisema Bunge hilo limetumia fedha nyingi za Watanzania ambazo zingeweza kuelekezwa katika shughuli za miradi ya maendeleo.
Chanzo: Nipashe
0 comments:
Post a Comment