Na Renatus Mahima, Tabora
MABINGWA watetezi, Yanga SC wamezinduka baada ya kuwachapa mabao 3-0 wenyeji Rhino Rangers katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara iliyochezwa katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora
Shujaa wa Yanga SC, leo alikuwa ni mshambuliaji Jerry Tegete aliyefunga mabao mawili moja kila kipindi, wakati lingine lilifungwa na Hussein Javu kipindi cha pili.
Yanga SC sasa inatimiza pointi 43 baada ya mechi 20 na kuendelea kubaki nafasi ya pili, nyuma ya Azam FC yenye pointi 44 baada ya kucheza mechi 20 pia.
Shujaa; Jerry Tegete kushoto leo ameifungia Yanga SC mabao mawili Tabora |
Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm alifanya mabadiliko katika safu yake ya ushambuliaji leo akiwaanzisha pamoja Mrisho Ngassa na Tegete badala ya Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza, wakati Emmanuel Okwi na Simon Msuva walikuwa wakishambulia kutokea pembezoni mwa Uwanja.
Tegete aliifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya 30 kwa shuti kali akiwa ndani ya eneo la hatari baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Charles Mpinuki kufuatia mchomo mkali wa kiungo Hassan Dilunga.
Kipa Juma Kaseja aliokoa michomo ya hatari ya Rhino katika dakika za 27, 42 na 45, wakati Dilunga mbali na shuti lililorudishwa na kipa kabla ya kujazwa nyavuni na Tegete, pia aligongesha mwamba mara mbili dakika za 20 na 26.
Kipindi cha pili, Yanga SC waliendelea kulishambulia lango la Rhino na dakika ya 69, Tegete tena alifunga bao la pili baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa timu hiyo ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kufuatia krosi ya winga Simon Msuva. Mpira huo ulimparaza beki Laban Kambole wakati unatinga nyavuni.
Hussein Javu aliyetokea benchi dakika ya 79 kuchukua nafasi ya Tegete, aliifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 90 akiitendea haki pasi nzuri ya Okwi nje kidogo ya lango la Rhino.
Huu unakuwa ushindi wa kwanza kwa Yanga SC ndani ya mechi tatu za Ligi Kuu, baada ya kulazimishwa sare mbili mfululizo na Mtibwa Sugar 0-0 mjini Morogoro na Azam FC 1-1 mjini Dar es Salaam, mechi zote wapinzani wake wakiwa pungufu ya mchezo mmoja baada ya kadi nyekundu.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Jerry Tegete/Hussein Javu dk79, Mrisho Ngassa na Emmanuel Okwi.
Rhino Rangers; Charles Mpinuki, Julius Masunga, Ally Mwanyiro, Abdallah Said, Laban Kambole, Msafiri Hamisi, Hussein Abdallah, Mussa Digubike, Gideon Brown, Rajab Twaha na Suleiman Jingo/Abbas Mohammed dk79.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo leo, JKT Ruvu imefungwa mabao 2-0 na Mbeya City Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam, mabao yote yakitiwa kimiani na Saad Kipanga dakika za tisa na 69. Mbeya City inatimiza pointi 42 baada ya mechi 22 na kuendelea kubaki nafasi ya tatu.
Kwa hisani ya Bin Zubeiry blog
Kwa hisani ya Bin Zubeiry blog
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi nne, Simba SC wakimenyana na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam FC itaonyeshana kazi na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Azam Complex. Mechi hizo mbili zitakuwa ‘live’ kupitia Azam TV.
Mechi nyingine za Jumapili ni Mgambo Shooting dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, wakati Ruvu Shooting na Ashanti United zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
0 comments:
Post a Comment